The House of Favourite Newspapers

Cuba Kuanza Kupata Internet Kwenye Simu Zao

WANANCHI wa Cuba wataweza kupata mawasiliano ya Internet kwenye simu zao kuanzia kesho (Alhamisi), kwa mujibu wa shirika la simu la serikali (ETECSA), hali ambayo itaiondoa nchi hiyo katika tatizo la kutengwa kimawasiliano kwa miaka mingi.

Karibu nusu ya wakazi milioni 11.2  wa nchi hiyo inayotawaliwa Kikomunist wana simu za mkono japokuwa si wote watakaoweza gharama ya kuwa na Internet kwenye simu zao.

Katika taarifa ya habari iliyotolewa jana, ETECSA ilitangaza vifurushi vya siku 30 vya kuanzia  MB 600 ambavyo vitalipiwa Dola 7 ( Sh. 16,000) na vya GB 4 Dola 30 (Sh.  69,000).  Kwa MB 100 gharama itakuwa Dola 10 (Sh. 23,000).

Gharama hizo zitakuwa ni kubwa mno kwa Wacuba wengi ambao wastani wa mishahara yao  serikalini ni Dola 30 (Sh. 69,000) kwa mwezi ambapo wengi wao hutegemea kutumiwa fedha na ndugu zao kutoka nchi za nje.

“Jambo hili lilibidi liwe limewezekana tangu zamani,” anasema mkazi wa jijini Havana, Joaquim Montiel (58) na kuongeza: “Lakini kwa watu kama mimi, bado jambo hilo liko mbali sana.”

 

Montiel anasema hataweza kununua simu ya teknolojia ya 3G kutoka katika mshahara wake ambao hauzidi Dola 20 kwa mwezi.

Cuba imekuwa nyuma sana katika masuala ya mitandao, aidha kwa kukosa fedha, vikwazo vya muda mrefu ilivyowekewa na Marekani au haja ya kutaka kudhibiti uingiaji wa habari nchini humo.

 

Comments are closed.