The House of Favourite Newspapers

DEREVA WA LISSU ASIMULIA “WALIVAA KOFIA NA MIWANI MYEUSI”

KWA mara ya kwanza, dereva wa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu aliyekuwa naye siku ya kushambuliwa kwake, Adam Bakari amesema shambulizi walilofanyiwa lilikuwa likijulikana na kutaka watu kutomhusisha na tukio hilo.

 

Adam ametoa kauli hiyo wakati akifanyiwa mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Ujerumani (DW) Deutsche Welle na kudai kuwa, licha ya eneo hilo kulindwa na askari wenye silaha kila siku, lakini siku ya tukio hilo Septemba 7, 2017 katika makazi ya mbunge huyo hakukuwa na ulinzi wa aina yoyote.

 

Mbunge huyo alishambuliwa kwa zaidi ya risasi 30 ambazo 16 zilimpata akiwa ndani ya gari, nyumbani kwake, Area D, jijini Dodoma lakini dereva huyo hakupatwa na risasi na Lissu mara kadhaa amekuwa akieleza jinsi alivyomsaidia kuokoa maisha yake.

 

“Mimi sikujificha baada ya tukio na tuliwaambia kama wanataka kunihoji waje Nairobi, Kenya lakini hawakufanya hivyo, licha ya muda wote niliokuwepo pale.


“Siku hiyo tulikuwa tukitokea bungeni kurudi katika eneo tunaloishi, ndipo nikagundua kwa nyuma kuna magari mawili yanatufuatilia, nilipoona yapo nyuma yetu kwa muda mrefu, nikaona bora niyapishe lakini hayakupita, nikaamua kukunja kona ya kwanza nikaona gari bado zipo, nikakunja kona ya pili zipo, nikaona hizi gari sio salama kwetu, hivyo nikaongeza mwendo.

 

“Wakati huo sikumwambia chochote bosi (Lissu). Tukafika karibu na nyumbani kuna ‘club’ inaitwa ‘84’ gari iliyokuwa inanifuatia mimi ni V8 (Toyota) ikapaki pembeni ile Nissan iliyokuwa nyuma yake ilikuja kwa speed (kasi) kunifuata mimi nilipoingia getini na yenyewe iliingia.”

 

“Tukapaki gari na wenyewe wakapaki wakiwa wamevaa kofia na miwani wakawa wanazungumza pale bila sisi kusikia. Walipomaliza gari ilirudi nyuma speed na ilipofika usawa wa gari yetu ilisikika tu milio ya risasi,” alisema Adam.

 

Alidai kuwa aliposikia kelele za milio ya risasi na kelele za Lissu aliyekuwa ameketi upande wa kushoto, alifungua mlango wa gari upande wa kulia na kumvuta mbunge huyo nje. Wakati akifanya jambo hilo risasi zilikuwa zikiendelea kumiminwa katika gari hilo, “mimi nilichanwa na vioo katika baadhi ya maeneo ya mwili wangu,” alisema Adam.

Comments are closed.