×

Dkt. Biteko: Tanzania Kujifunza Teknolojia Ya Magari Ya Umeme Singapore

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt Doto Biteko akishuka kwenye moja ya gari inayotumia umeme kutoka kwenye kiwanda cha magari cha HYUNDAI Motor Group ambayo ni rafiki kwa mazingira, mara baada ya kutembelea kiwanda hicho Oktoba 23, 2024 nchini Singapore.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, amesema kuwa Tanzania inayo nafasi kubwa ya kujifunza Teknolojia ya uwambaji wa magari (Assembling) yanayotumia umeme kutoka kiwanda cha magari cha HYUNDAI kwani ni rafiki kwa mazingira na hupunguza uchafuzi wa hali ya hewa.

Dkt. Biteko ameyasema hayo Oktoba 23, 2024 nchini Singapore mara baada ya kutembelea kiwanda hicho ikiwa ni ziara mojawapo kwenye mkutano wa Wiki ya Nishati nchini Singapore na kusema kuwa Teknolojia kama hizi zina mchango mkubwa kwenye kuinua uchumi wa nchi na kuongeza pato la Taifa.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akishuhudia moja ya teknolojia ya ubunifu kutoka kampuni ya Hyundai inayotumia teknolojia ya akili mnemba ili kuzalisha bidhaa za kilimo (Smart farm) Oktoba 23, 2024 nchini Singapore.

‘’ Nawapongeza sana wenzetu hasa kwa Teknolojia na ubunifu wa haya magari pamoja na Teknolojia ya Kilimo janja (smart farm) ambapo kwanza inatumia nafasi ndogo lakini matokeo yake ni makubwa sana’’ Alisema Dkt. Biteko.

Kuhusu Teknolojia ya kilimo janja ambacho kinaendeshwa na kampuni ya ubunifu ya HYUNDAI kwa kutumia Teknolojia mnemba (Robot) Dkt. Biteko amesema, uwepo wa Teknolojia kama hii unaongeza tija, inapunguza gharama kwenye uendeshaji wake.

Naye, Makamu wa rais na Mkuu wa Biashara na mipango kutoka HYUNDAI Motor Group amesema mafanikio hayo yanayokana na kutumia fursa iliyopo wakati wa changamoto zilizokuwepo awali kama ya matumizi ya mafuta kwenye magari ambapo haikuwa rafiki kwa mazingira pamoja na uhaba wa maeneo kwa ajili ya kilimo nchini Singapore.

Leave a Comment