The House of Favourite Newspapers
gunners X

Dkt. Rugemeleza Nshala Atimiza Miaka 30 ya Uwakili, Aeleza Safari Yake

0
Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wakili Dkt. Rugemeleza Nshala

Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wakili Dkt. Rugemeleza Nshala, Jumatatu Desemba 15, 2025 ametimiza miaka 30 tangu aapishwe rasmi kuwa Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama zote zilizopo chini yake, isipokuwa Mahakama ya Mwanzo.

Dkt. Nshala aliapishwa tarehe 15 Desemba 1995 na aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania wakati huo, Hayati Francis Nyalali, hatua iliyomfungulia rasmi mlango wa safari yake ya kitaaluma katika tasnia ya sheria ambayo sasa imedumu kwa miongo mitatu.

Katika kuadhimisha siku hiyo muhimu, Wakili Dkt. Nshala amechapisha andiko maalum kupitia mitandao ya kijamii, akisimulia kwa kina safari yake ya miaka 30 ya uwakili, changamoto alizokutana nazo pamoja na tafakuri juu ya nafasi ya sheria katika jamii.

 

Katika chapisho hilo, Dkt. Nshala ameandika:

“Mnamo tarehe 15 Desemba 1995 niliapishwa na Jaji Mkuu, Francis Nyalali, kuwa Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama za chini yake isipokuwa Mahakama ya Mwanzo. Leo imetimia miaka 30, ninasema asante kwa Mungu Mwenyezi kwa baraka na ulinzi wake kuweza kufanya kazi hii.”

Ameendelea kuwashukuru wateja wake wote waliomwamini na kumpa nafasi ya kuwatetea katika mashauri mbalimbali, akieleza kuwa katika safari yake ameshuhudia pande mbili za matumizi ya sheria.

“Nimeona mengi; jinsi sheria ikitumika vizuri ni chombo cha ukombozi na pale haki inapopindishwa basi ni chombo cha unyanyasaji na dhuluma,” ameandika.

Aidha, Dkt. Nshala amesisitiza wajibu wa mawakili katika kuhakikisha haki inatendeka na kuilinda Mahakama kama muhimili huru wa dola, bila kuingiliwa na mihimili mingine, hususan muhimili wa utendaji wa Serikali.

Kutokana na changamoto za kisheria na kikatiba anazoziona kwa sasa, Wakili huyo mkongwe ametoa wito wa kuandikwa upya kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akieleza kuwa mgawanyiko mkubwa uliopo umefanya mabadiliko ya katiba kuwa jambo lisiloepukika.

KWA UCHUNGU RAIS SAMIA AWAFUNDA JWTZ “MSITUMIKE KWA MATAMKO”, KESI YA LISSU BADO NGOMA NGUMU

Leave A Reply