×

Enoch Sontonga: Mtunzi wa Wimbo wa Taifa Tanzania

Enoch Sontonga Mtunzi wa Wimbo wa Taifa Tanzania

Mungu Ibariki Afrika ni jina la Wimbo wa Taifa wa Tanzania. Asili yake ni Wimbo wa Nkosi Sikelel’i Afrika wa Afrika Kusini. Enoch Sontonga ndiye mtunzi wa Nkosi Sikelel’i Afrika mwaka 1897 hata kabla ya nchi nyingi za Afrika kupata uhuru.

Sehemu ya wimbo huu inatumika pia katika nyimbo za taifa za Afrika Kusini na Zambia. Na huko nyuma ulitumiwa kama Wimbo wa Taifa wa Zimbabwe.

Sontonga alizaliwa mwaka 1873 na kufariki Aprili 18, 1905.
Hata kabla ya TANU (Tanganyika African National Union), kuanzishwa mwaka wa 1954, wimbo huo, Nkosi Sikelel’ iAfrika, ulikuwa unaimbwa Afrika Kusini.

Chama cha Afrika Kusini, African National Congress (ANC), kilianzishwa miaka mingi kabla ya chama cha TANU. Na kwenye mkutano wa kwanza uliofanyika Bloemfontein, Afrika Kusini, wakati wa kuanzisha chama hicho mwaka wa 1912, waliimba Nkosi Sikelel’ iAfrika.  Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa bado hajazaliwa wala chama cha TANU.

Chama cha kule Afrika Kusini kilichoanzishwa mwaka wa 1912 kiliitwa South African Native Congress chini ya uongozi wa John Dube, Mzulu na Pixley ka I. Seme kikabadilishwa jina baadaye na kuitwa African National Congress (ANC).
Kuanzia mwaka wa 1925, wana ANC waliuchagua wimbo huo, Nkosi Sikelel’ iAfrika, kama wimbo wao wa taifa na unaimbwa hadi leo.
Katika nyimbo za mataifa yetu ya Kiafrika, hakuna wimbo mwingine unaojulikana kama wimbo huo.

Enoch Sontonga alitoka Eastern Cape Province, Jimbo la Wakosa (Xhosa), ambako pia ni nyumbani kwa Nelson Mandela. Alitunga wimbo huo katika lugha yake ya Kikosa na alitunga kama wimbo wa kanisa.

Alipotunga wimbo huo mwaka wa 1897, haukuimbwa hadharani mpaka mwaka wa 1899. Uliimbwa kanisani kwa mara ya kwanza mwaka huo.
Halafu, baada ya miaka 13, uliimbwa kwenye mkutano wa kwanza wa South African Native Congress mwaka wa 1912 uliofanyika Bloemfontein Afrika Kusini kilipoanza kugombea haki za Wafrika.

Hata Watanganyika wengi waliokwenda kufanya kazi migodini Afrika Kusini miaka ya 1940 na 1950 waliujua wimbo huo. Walikuwa wanaimba Nkosi Sikelel’ iAfrika pamoja na watu wa Afrika Kusini walipokuwa huko na waliporudi Tanganyika.

Wote wenye music sheets za wimbo huo, wanaweza kukuonesha jina la Enoch Sontonga kama ndiye mtungaji wa wimbo huo.
Ulikuwa katika lugha mbili, Kiswahili na Kiingereza na kichwa chake kilikuwa ni God Bless Africa, yaani Nkosi Sikelel’ iAfrika (Mungu Ibariki Afrika).

Melody ya Nkosi Sikelel’ iAfrika ukiisikiliza hutaona tofauti hata kidogo na melody ya wimbo wetu wa taifa,  au melody ya wimbo wa taifa kule Zambia.

Kama nilivyosema kabla, wimbo huo siyo wa watu wa Afrika Kusini tu. Enoch Sontonga aliandika na alitunga wimbo huo kama ni wimbo wa bara lote. Ndiyo maana alisema Nkosi Sikelel’ iAfrika, yaani God Bless Africa na siyo God Bless South Africa.

Nyimbo zake nyingi alizotunga zilikuwa ni nyimbo za huzuni kuhusu maisha magumu ya Waafrika chini ya utawala wa Wazungu waliokuwa wanawakandamiza Waafrika katika bara lote.
Wimbo wake, Nkosi Sikelel’ iAfrika, ulitokana na maumivu hayo ya Waafrika ingawa pia ulikuwa ni wimbo wa kuwapa tumaini kwamba hawako peke yao kwani Mungu yuko nao, au yuko nasi, ingawa tulikuwa tunateswa na wakoloni toka Ulaya.

Wimbo huo, Nkosi Sikelel’ iAfrika, uliwekwa kwenye sahani ya santuri kwa mara ya kwanza, London, mwaka wa 1923. Uliimbwa na Solomon Plaatje, mwimbaji maarafu wa Afrika Kusini ambaye pia alikuwa ni mmoja wa Waafrika walioanzisha chama cha South African Native Congress.

Kwa hiyo hatukuiba na hatukuazima, wimbo huo. Ni wetu kama wao kule Afrika Kusini na nchi zingine. Na Enoch Sontonga alitambuliwa kwenye music sheets za wimbo huo nchini Tanganyika na baadaye Tanzania, kama ndiyo mtungaji wa God Bless Africa.
Utumizi wetu wa wimbo huo,  unaonesha pia umoja na undugu wetu kama Waafrika. Ndiyo maana kulikuwa na vyama vilivyopigania uhuru ambavyo majina yao yalifanana au yalikuwa karibu sana.

Kwa mfano, African National Congress (ANC) iliyoundwa Tanganyika na kuongozwa na Zuberi Mtemvu na katibu wake mkuu John Chipaka ilikuwa na jina sawa na la chama cha Afrika Kusini cha akina Nelson Mandela na wenzake.

ANC ilikuwepo pia Northern Rhodesia (Zimbabwe) kilichoongozwa na Harry Nkumbula na kiliendelea kuitwa hivyo hata baada ya wanachama wengine kuondoka na kuunda chama kingine, United National Independence Party (UNIP), chini ya uongozi wa Kenneth Kaunda.
Majina hayo, katika nchi zetu mbalimbali, yanafanana kwa sababu tunajiona kama ni ndugu na ni kweli sisi sote ni ndugu. Ni sawa na wimbo wa Nkosi Sikelel’ iAfrika kuwa Wimbo wa Taifa Tanzania, Zambia na South Africa.

Leave a Comment