The House of Favourite Newspapers

Falcao, Balinya Wampasua Kichwa Zahera

David Molinga ‘Falcao’.

IKIWA katika maandalizi yake ya mwisho kuelekea mechi ya kimataifa, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ameendelea kupambana kutengeneza kombinesheni kwa wachezaji wake ili kuwa na kikosi imara.

 

Zahera amekuwa akifanya kazi hiyo katika kambi ambayo Yanga iliweka visiwani Zanzibar ambapo leo Ijumaa inatarajiwa kurejea hapa Dar tayari kwa mchezo wao dhidi ya Township Rollers katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Katika kikosi chake, washambuliaji ni pamoja na David Molinga ‘Falcao’, Juma Balinya, Sadney Urikhob na Maybin Kalengo. Akizungumza na Championi Ijumaa, Mratibu wa Yanga, Hafidhi Saleh, alisema kuwa kocha anapambana kuona anapata kombinesheni nzuri kwa wachezaji wake ambao kwa asilimia kubwa kikosi chake bado ni kipya kutokana na wachezaji wapya.

 

“Unajua kocha kwa sasa hivi kitu kikubwa ambacho anapambana nacho ni kuona kuwa anapata kombinesheni nzuri hasa kule mbele (mastraika), ili kuona timu inapata matokeo na kama unavyoona tuna majukumu muhimu ya kimataifa.

Juma Balinya

“Ndiyo maana kuna maeneo anayafanyia kazi zaidi kwa siku hizi chache ambazo tupo Zanzibar hapa, ukiangalia hata mechi yetu ile na Mlandege unaona kabisa alikuwa anajaribu kutengeneza kitu.

 

“Hata hivyo, kesho (leo) Ijumaa tutakuwa tunarejea Dar kufanya maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo wetu wa Ligi ya Mabingwa na Township Rollers,” alisema Hafidhi. Ikumbukwe katika mchezo wa juzi dhidi ya Mlandege, mbele aliwatumia Sadney, Balinya na Sibomana ambao wote watatu walifunga kwenye mchezo huo.

Comments are closed.