GSM yazima hujuma za Simba SC

KAMPUNI ya GSM ambao ni wauzaji wa jezi za Yanga, leo wanaingiza mzigo mpya wa jezi huku kukiwa na punguzo kubwa la bei katika kuelekea mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hiyo, ni habari njema kwa mashabiki wa Yanga katika kuelekea mchezo wao huo utakaopigwa Septemba 14, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 

Itakuwa mara ya tatu kwa Yanga kuleta jezi hizo baada ya kwanza kuleta na kumalizika kabla ya hivi karibuni kuleta tena zikiuzwa kwa Shilingi 35,000 kwenye maduka ya GSM.

 

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya uongozi wa Yanga, mzigo mkubwa wanaleta GSM unaoingia leo zitauzwa kwa Shilingi 30,000 badala ya 35,000 zitakazokuwa toleo la kwanza.

 

Chanzo hicho kilisema mzigo toleo la pili zitafika Jumatatu ijayo ambazo zitauzwa kwa Shilingi 20,000 na lengo ni kuona mashabiki wanazinunua kwa wingi katika mchezo wao zaidi ya Zesco ili kuvunja hujuma na fitna za watani wao Simba ambao wanajipanga kuingia na uzi wa Zesco Taifa Jumamosi ijayo.

 

Kiliongeza kuwa awali jezi hizo ziliuzwa bei kubwa kutokana na uharaka wa kufika na kulazimika kusafirisha na ndege ili zianze kuvaliwa na wachezaji kwenye kilele cha Wiki ya Mwananchi.

 

“Kesho (leo) zitaingia jezi toleo la kwanza zitakazoanza kuuzwa kwenye maduka ya GSM na kwa mawakala wetu kwa bei ya Shilingi 30,000 badala ya 35, 000 zilizokuwa zinauzwa awali.

 

“Na jezi toleo la pili zitaingia Jumatatu ya wiki ijayo toleo la pili zitakazouzwa kwa Shilingi 20,000 pekee na lengo ni kuona mashabiki wanazinunua jezi hizo kwa wingi ili wazivalie siku ya mchezo wetu na Zesco.

 

“GSM imefanya hivyo ili kuzuia fitna za Simba walizozipanga kufika uwanjani wakiwa na jezi zao na za Zesco, hivyo wameliona hilo na kuchukua maamuzi ya haraka ya kuzileta jezi hizo zitakazouzwa kwa bei ndogo,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela kuzungumzia hilo alikiri mzigo mpya huo wa GSM kutua nchini wakati wowote kuanzia kesho (leo).

 

“Tunafahamu kila kitu ambacho wanakifanya wapinzani wetu, hivyo kama uongozi tayari tumejipanga kupangua mipango yao yote, kikubwa mashabiki wajitokeze kwa wingi uwanjani wakiwa na jezi zao kwa lengo la kuujaza uwanja,” alisema Mwakalebela.

Said Ally, Dar es Salaam


Loading...

Toa comment