Haya Husababisha Mwanamke Kukosa Hedhi (Amenorrhea)
WANAWAKEwengi wamekuwa wakikosa hedhi na hali hiyo imekuwa ikiwaletea usumbufu mwingi wa kisaikolojia kwa waliowahi kukumbana na tatizo hilo.Tatizo la kukosa hedhi au kitaalamu amenorrhea linaweza kutokea awali kabisa (primary) au baadaye kabisa maishani.
Primary amenorrhea ni hali ya kukosa hedhi inayoweza kumtokea msichana aliye katika umri wa kuvunja ungo na ambayo huweza kuendana na hali ya kukosa mabadiliko ya kubalehe kama vile kuota matiti, au msichana anaweza kuwa na mabadiliko ya kubalehe lakini asipate hedhi.
Tatizo hilo likitokea baadaye kitaalamu Secondary amenorrhea ni hali ya kukosa hedhi inayomtokea mwanamke ambaye si mjamzito, hanyonyeshi na ambaye hajavuka umri wa kukosa hedhi kitaalamu menopause na wala hatumii njia za uzazi wa mpango kama vile sindano au vidonge na ambaye hapo awali alikuwa akipata hedhi kama kawaida lakini akasimama kwa miezi mitatu au zaidi.
Ili mwanamke aweze kuwa na mzunguko ulio sahihi wa hedhi, ni lazima matezi yake (ya hypothalamus na pituitary) pamoja na kiwanda cha kutengeneza mayai ya kike (ovaries) na mji wa mimba (uterus) vifanye kazi zake sawasawa.
Hypothalamus huchochea tezi la pituitary kuzalisha homoni chochezi ya follicle au follicle-stimulating hormone (FSH) pamoja na homoni ya luteinizing (LH). Hizi FSH na LH kwa pamoja huchochea ovaries kuzalisha homoni za estrogen pamoja na progesterone.
Kazi za estrogen na progesterone ni kusababisha mabadiliko katika ukuta wa uterus yaani endometrium ikiwepo kupata hedhi.
Ili damu ya hedhi iweze kutoka nje, njia ya uzazi ya mwanamke haina budi kuwa huru yaani isiyo na matatizo yoyote yale.Tujiulize, amenorrhea husababishwa na nini? Visababishi vya amenorrhea vyaweza kugawanywa katika makundi makuu matatu, vile vinavyohusisha matatizo katika mfumo wa homoni, vile vinavyohusisha matatizo ya kimaumbile katika njia ya uzazi ya mwanamke na vile vinavyohusisha mabadiliko katika mwili wa mwanamke.
Matatizo katika mfumo wa homoni: Matatizo katika mfumo wa homoni yanaweza kuwa katika tezi za hypothalamus, pituitary au ovary.Matatizo katika Hypothalamus yanayoweza kusababisha mwanamke kukosa hedhi ni pamoja na uvimbe katika ubongo karibu na tezi ya pituitary, ukosefu au upungufu wa homoni zinazochochea kukua na kufanya kazi kwa via vya uzazi. Ugonjwa huu hujulikana kama Kallmann syndrome.
Lishe duni na utapiamlo, uzito mdogo kuliko kawaida (kukonda kwa kupitiliza) na matatizo katika tezi ya Pituitary husababisha mwanamke kukosa hedhi.Vyanzo vinavyohusisha tezi ya pituitary ni pamoja na kuwepo kwa kiwango kikubwa cha homoni ya prolactin katika damu au kwa kitaalamu Prolactinemia.
Prolactin ni homoni inayochochea uzalishaji wa maziwa kwenye matiti ya mama wakati wa kunyonyesha.
Hali ya kuwa na prolactin nyingi katika damu inaweza kutokea iwapo kuna uvimbe unaoitwa prolactinoma katika tezi ya pituitary, kuwepo kwa uvimbe mwingine wowote katika tezi ya pituitary, Pituitary kushindwa kufanya kazi baada ya seli zake kufa, hususan iwapo mama alipoteza damu nyingi wakati wa kujifungua.
Kuharibika kwa tezi ya pituitary baada ya seli zake kushambuliwa na mfumo wa kinga ya mwili na kuwa na historia ya kupata tiba ya mionzi inayohusisha tezi ya pituitary husababisha kukosa hedhi.Vyanzo vinavyohusisha matatizo katika viwanda vya kuzalisha mayai ya kike yaani ovaries ni pamoja na kutozalishwa kabisa kwa mayai (Anovulation), kuwepo kwa kiwango kingi cha homoni za kiume katika damu (Hyperandrogenemia, ovary kuwa na vifukovifuko kitaalamu Polycystic ovarian syndrome na kushindwa kufanya kazi zake vizuri.
Haya ni matatizo ya homoni ambayo huwapata baadhi ya wanawake walio katika umri wa kuzaa naovary kushindwa kufanya kazi kabla ya muda wake.Msichana kushindwa kuvunja ungo na msichana kuwa na kimo kifupi kuliko kawaida husababisha msichana kupata hedhi.
Historia ya kuwahi kupata tiba ya mionzi au madawa yanaathiri ovary, ugonjwa wa kurithi wa Galactosemia unaoambatana na kuwa na kiwango cha juu cha sukari aina ya galactose katika damu na husababisha tatizo hili.