Historia Yaandikwa New York Meya wa Kwanza Mwislamu Aanza Kazi

Zohran Mamdani ameanza rasmi kazi yake kama Meya wa Jiji la New York, akiahidi kuubadili utendaji wa serikali ya jiji kwa ajili ya wananchi wanaohangaika na gharama kubwa za maisha.
Mamdani, ambaye ni mwanachama wa chama cha Democratic na anajitambulisha kama “mdemokrati wa kijamaa,” aliapishwa muda mfupi baada ya saa sita usiku katika kituo cha treni ya chini ya ardhi kilichoachwa chini ya City Hall—akiwa meya wa kwanza Mwislamu katika historia ya jiji hilo.
Katika kiapo hicho cha usiku wa manane, aliweka mkono wake juu ya Qur’an, ishara iliyotajwa kuwa ya kipekee katika uongozi wa jiji lenye wakazi zaidi ya milioni nane.
Baada ya kufanya kazi kwa sehemu ya usiku katika ofisi yake mpya, Mamdani alirejea City Hall mchana kwa hafla kubwa ya hadhara, ambapo Seneta Bernie Sanders alimsimamia kiapo kwa mara ya pili.
“Kuanzia leo, tutatawala kwa upana na kwa ujasiri. Huenda tusifanikiwe kila mara, lakini hatutawahi kushutumiwa kwa kukosa ujasiri wa kujaribu,” alisema Mamdani mbele ya umati ulioshangilia.
Stori na Elvan Stambuli, Global

