JEURI KAMA YOTE, DIMPOZ AWAVIMBIA KIBA, MONDI

DAR ES SALAAM: Dunia inakwenda kasi sana na ni vigumu mno kuisimamisha! Miezi kadhaa baada ya afya yake kuyumba kisha kulazwa hospitali mbalimbali nje ya nchi ikiwemo Afrika Kusini, Ujerumani na Kenya, staa mkubwa wa Bongo Fleva, Omary Faraji Nyembo almaarufu Ommy Dimpoz ameonesha jeuri kama yote, Amani limedokezwa. 

 

Dimpoz, baada ya kufanyiwa operesheni ya koo kwa kunyweshwa kitu kilichodaiwa ni sumu, watu wengi akiwemo mchekeshaji Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ waliamini hataweza tena kurejea kwenye gemu na kuimba kama awali kisha kukimbiza kwa mafanikio kwenye muziki wa Bongo Fleva.

 

Lakini fumba na kufumbua, waliokuwa hawaamini wakashangaa kumuona Dimpoz huyu hapa, amerejea kwenye mstari kwa kishindo. Siyo kurejea tu, lakini akarejea na makali yaleyale ya kwenye nyimbo zake za mwanzo kama Nai Nai, Me and You, Baadaye, Nani Kama Mama na nyinginezo.

AWAVIMBIA KIBA, MONDI

Baada ya kurejea, uchunguzi wa Gazeti la Amani umebaini kwamba, sasa Dimpoz anawavimbia washindani wake kwenye gemu akiwemo bosi wake, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ na aliywahi kuwa swahiba wake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ au ‘Mondi’. Ndani ya kipindi kifupi baada ya kupona, Dimpoz ameachia nyimbo mbili za Ni Wewe na You Are The Best.

 

NYIMBO ZAKE ZAKIMBIZA

Hadi mapema wiki hii, Ni Wewe ulikuwa na watazamaji zaidi ya milioni mbili kwenye Mtandao wa YouTube huku You Are The Best ukiwa na watazamaji zaidi ya milioni 1.5 hivyo kukimbizana na Kiba na wimbo wake wa Kadogo uliokuwa na watazamaji zaidi ya milioni 5 na Inama wa Mondi (audio) uliokuwa umesikilizwa na zaidi ya watu milioni 2.

AKIMBIZA KWA SHOO

Kwa ngoma hizo mbili tu, Dimpoz akaanza kukimbiza upya kwa shoo za ndani na nje kisha kuanza kutengeneza mkwanja kama wanavyofanya Kiba na Mondi. “Hakuna jambo alilokuwa analitamani Dimpoz kama kurejea kwenye gemu na kuona akifanya vizuri hasa kwenye eneo la shoo,” anasema mmoja wa mameneja wa Dimpoz, Aidan Seif.

 

“Ningemchangia rafiki yangu Jojo (Jokate Mwegelo, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe) kiasi kikubwa, lakini kama mnavyojua nilikuwa ninaumwa na shoo hakuna,” alisema Dimpoz kwenye Harambee ya Tokomeza Zirro iliyoendeshwa na Jokate hivi karibuni kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar. “Lakini sasa Mungu ni mkubwa, jamaa (Dimpoz) anakula shoo na kukimbizana na kina Kiba na Mondi,” anasema mtu wa karibu wa Dimpoz kwa sharti la kufichwa jina.

AVUTA RANGE ROVER

Katikati ya kipindi kifupi cha mafanikio, tayari Dimpoz amevuta ndinga kali aina ya Range Rover Sport na kuliongeza kwenye maegesho nyumbani kwake Mikocheni jijini Dar ambako kulikuwa na gari lake la zamani aina ya Toyota Prado.

 

Wakati Dimpoz akinunua gari hilo la kifahari aina ya Range Rover Sport, Kiba anaendelea kusukumu gari lake la kitambo aina ya BMW X5 huku Mondi akiwa na Toyota Land Cruiser V8 na BMW X6. Baada ya kulinunua gari hilo likiwa na rangi nyeupe, Dimpoz alilibadilisha na kuwa na rangi ya chungwa kisha kuli-pimp na kuwa la kistaa zaidi.

 

MENEJA ATHIBITISHA

Ili kuthibitisha umiliki wa gari hilo, Gazeti la Amani lilizungumza na mmoja wa mameneja wake, Aidan Seif ambaye alithibitisha kuwa ni mali yake. “Kuhusu gharama yeye mwenyewe ndo’ anajua, lakini kuhusu kulimiki, ni kweli ni gari lake analomiliki kwa sasa,” alisema Aidan.


Loading...

Toa comment