The House of Favourite Newspapers

Kali ya Mwaka! Bibi Noma, Awahenyesha Polisi Wenye Silaha Nzito

MOROGORO: Shubaamit! HIVI ukitazama picha ukurasa wa mbele unaweza kufikiria nini hasa? Vyovyote utakavyofikiri; mwisho wa picha duniani kuna mambo na kuishi kwingi ni kuona mengi.

Kasheshe iliyotokea hivi karibuni kwenye Kituo cha Polisi cha Kata ya Mji Mpya mjini hapa, kati ya polisi na mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Bibi Kibena ni ya aina yake, Amani lilikuwepo eneo la tukio.

Kwanza ni jinsi mwanamke huyo alivyotinga kituoni hapo. Pili, madai na vitisho vyake kwa mwandishi na wanausalama. Tatu, pilikapilika ya kumuondoa kituoni hapo ilivyokuwa. Nne, gumzo aliloliacha eneo la tukio na hitimisho lake.

 

TUANZE HABARI

Mwanzoni mwa wiki hii ambapo mfungo wa mwezi mtukufu ukiwa umeanza asubuhi na mapema, Bi Kibena alionekana ameketi mbele ya kituo hicho cha polisi, asijulikane alifikafikaje pale; kilichotokea kwa mashuhuda ni mshangao tu.

Pengine kwa kujua kila ugeni huambatana na utambulisho, polisi walipofika kituoni na kumkuta walimuuliza Bi Kibena kulikoni asubuhi ile kuwatembelea akiwa na vazi jeusi maarufu kama kaniki?

Polisi: Unaitwa nani?

Bi Kibena: Unataka nini, wewe hujui nimefikaje hapa?

Wakati askari wa zamu akiandaa cha kuuliza Bi Kibena alianza kutoa angalizo lenye onyo kwamba hataki mjadala wowote kati yake na wenyeji wake, vinginevyo ‘angekinukisha’.

 

POLISI WENGINE WAITWA

Baada ya mahojiano hayo kuonekana yamejaa lugha gongana yenye kufikirisha na wakati mwingine kutia hofu itokanayo na wenyeji kujiuliza ‘huyu ni nani?’, hatua ya kuongeza nguvu kwa kuitwa askari wengine waliokuwa wakifanya doria mitaani ilichukuliwa haraka.

Kama ijulikanavyo mambo ya kijeshi hayana kulemba; fumba jicho fumbua polisi wengine wawili walifika eneo la tukio, kwa ujasiri waliuliza kuna nini? Kabla hawajashibishwa maelezo yamhusuyo Bi Kibena, waliamua kumvaa.

Polisi: We mama unafanya nini hapa?”

Bi Kibena: (Kimya tu, aliwatolea macho yaliyoonesha ishara ya ujeuri wa kutisha.)

Polisi: Hutaki kujibu eee!

Bi Kibena: Unakuja kwangu na bunduki, unaweza kunitisha mimi kwa lipi…

Polisi: Hakuna anayekutisha…(Bi Kibena hakutaka kusikiliza maelezo.)

Bi Kibena: Angalia ile milima ya Ulugulu, hivi kati yako na ile milima nani alikuwa wa kwanza kuwepo hapa duniani?

Bila shaka hata ungekuwa wewe msomaji, swali hili lingekuwa gumu kupatiwa majibu na ndivyo ilivyokuwa kwa polisi aliyekuwa anamhoji mwanamke huyo ambapo ulingo wa mikwara aliendelea kuutawala yeye.

Bi Kibena: Usijaribu kufanya kitu chochotea nitakufanya vibaya, na wewe mwanadishi unayejifanya kupigapiga picha kesho hutaamka.

 

RIPOTI YATUMWA MAKAO MAKUU

Inawezekana isiwe sawa kwa polisi waliokuwepo eneo la tukio kuamini kama mkwara wa Bi Kibena uliwatikisa lakini kitendo cha wao kufikisha habari zake kituo kikuu cha polisi mjini hapa na baadaye askari wengine sita kutumwa eneo la tukio, unaweza kupata kiimani flani kwamba nao walitii sheria bila shuruti.

Aidha, hata baada ya polisi wale sita wakiwa na silaha za moto kufika eneo hilo la tukio na kukuta umati ukiwa umemzunguka Bi Kibena, haikuwa kazi rahisi kuchukua na kumpeleka kituo kikuu cha polisi.

Bi Kibena: Siwezi kuondoka hapa hivihivi, ninachotaka basi la ….(analitaja jina basi linalomilikiwa na kampuni kubwa ya usafirishaji hapa nchini) lije hapa linichukue.

Polisi: Utakwenda kupanda huko tuendako, tuliite hapa basi kubwa gharama zake utalipa wewe?

Bi Kibena: Gharama ndiyo kitu, eee, unadhani mimi nashindwa kulipia…liite hapa uone.

Polisi walipoona mikwara ya Bi Kibena inazidi na hakuna walichofanikiwa kukifahamu kwake zaidi ya hilo jina na mahali atokapo kwa maana ya Mikese nje kidogo ya mji, waliamua kuacha kazi wafanye kazi.

Waliotazama shoo ya polisi na Bi Kibena hata kama hawakuilipia chochote lakini waliinjoi kwa namna fulani ambapo kwako wewe msomaji unaweza kujionea sehemu ya tukio hilo kwa kutazama picha zilizotumika ukurasa wa kwanza.

Waswahili husema, hakuna mkate mgumu mbele ya chai, baada ya timbwili, Bi Kibena aliufyata, akapandishwa kwenye gari tayari kupelekwa kituo kikuu.

 

BI KIBENA NI NANI?

Kwa sababu aligoma kujielezea yeye ni nani, kazi ya kumtambua inakuwa ngumu, lakini ukweli unabaki kuwa si mtu wa kawaida ukimtazama.

Wapo baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walifika mbali kwa kumhusisha Bi Kibena na imani za ushirikina lakini Amani haliamini katika hilo na kwamba linaendelea kufuatilia kitaalamu ili kujua hali yake halisi.

MWENYEKITI ATIA NENO

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Fumilwa, Kitukwa Chabala aliyekuwepo eneo la tukio alithibitisha kutokea kwa tukio hilo kwenye eneo lake.

“Hiki kituo cha polisi kipo kwenye mtaa wangu, huyu bibi yawezekana ni mwanga maana matendo yake si ya kawaida,” alidai Chabala.

 

RAI YA AMANI

Siku za hivi karibuni kumekuwepo na matukio ambayo jamii imekuwa ikiyahusisha na imani za kishirikina na hatimaye kuleta maafa, jambo ambalo katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia ni vema imani hizo zikawekwa kando.

Mara kadhaa imeshuhudiwa baadhi ya watu wakipigwa na wananchi wenye hasira na kuuawa kwa madai kuwa ni wanga lakini baadaye hutambulika kuwa na matatizo ya akili, jambo ambalo linatajwa kudhulumu haki yao ya kuishi. Sote tukemee imani za kishirikina.

Stori: Dunstan Shekidele, Amani

Comments are closed.