Kipa mpya Yanga atua Dar kininja

Metacha Mnata.

HADI kufikia leo Ijumaa jioni viongozi wa Yanga watakuwa wanamtangaza staa mwingine mpya klabuni hapo. Huo ni mwendelezo wa kujiweka sawa kwa ajili ya msimu ujao wa 2019/20 baada ya kuyumba kwa muda mrefu, sasa kasi yao katika usajili inamaanisha kuwa hawataki utani.

 

Mchezaji huyo ni kipa Mtanzania Metacha Mnata ambaye anatarajiwa kuwa mbadala mpya wa aliyekuwa kipa wao, Beno Kakolanya baada ya pande hizo mbili kumalizana kwa kila kitu.

 

Yanga wanatarajia kumtambulisha Metacha kuwa kipa wao mpya kwa msimu ujao baada ya klabu hiyo kumtumia tiketi ya ndege na kumleta Dar es Salaam kwa ajili ya kumsainisha mkataba.

 

Metacha anatua Yanga akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza muda wake katika timu ya Mbao FC aliyokuwa akiitumikia kwa mkopo kutoka Azam FC. Meneja wa kipa huyo ambaye hakutaka kuandikwa gazetini ameliambia Championi Ijumaa, kuwa leo Ijumaa watakutana na vigogo wa Yanga kwa ajili ya kuzungumza mara ya mwisho kabla ya kusaini mkataba.

 

“Mazungumzo yapo vizuri kwa kila kitu, sasa tuko asilimia 95 za Metacha kujiunga na Yanga na kesho (leo) Ijumaa tunamaliza mazungumzo ya mwisho kisha tutaingia mkataba.

 

“Metacha ameshakuja Dar baada ya kutumiwa tiketi ya ndege na viongozi hao wa Yanga, kila kitu kuhusiana na dili hilo basi hadi kufikia hiyo Ijumaa kitaanikwa wazi,” alisema meneja huyo.

 

Kwa upande wake, Metacha ambaye amefikia katika sehemu moja ambayo ametulia kwa muda akiwa hatakiwi kuwa na makeke mengi mjini, jina la eneo likiwekwa kapuni kutokana na sababu maalum, ameliambia Championi Ijumaa, kuwa tayari yupo Dar kwa ajili ya kuwasikiliza Yanga kabla ya kumalizana nao.

 

“Nipo Dar, ambapo nimekuja kuwasikiliza Yanga, kila kitu kinaenda sawa na kama tutafikia makubaliano basi nitasaini kwao.”

USAJILI : MASHINE Zilizotua YANGA Usiku, SIBOMANA ,BIGIRIMANA Ndani!!

Loading...

Toa comment