The House of Favourite Newspapers

Kiungo Simba: Yanga wamenasa Jembe

SIKU chache baada ya kudaiwa kuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera anatarajiwa kumchukua kiungo mshambuliaji wa timu ya Kariobang Sharks ya Kenya, Duke Abuya, usajili huo umepongezwa kuwa ni muafaka kwa klabu hiyo.

 

Sifa hizo zimemwagwa kwa Abuya kuwa anaweza kuwa msaada mkubwa kwa Yanga ikiwa kila kitu kitaenda safi. Abuya ambaye aliitesa Yanga katika mashindano ya SportPesa Super Cup ambayo yalifanyika hapa nchini Januari, mwaka huu kwa kuifungia mabao mawili katika ushindi wa mabao 3-2 wa timu yake, anadaiwa kusaini mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia timu hiyo kuanzia msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa katika mahojiano maalum, kiungo wa zamani wa Simba, Jerry Santo, raia wa Kenya, alisema kuwa kama Zahera amefanikiwa kuipata saini ya Abuya basi atakuwa amelamba dume.

 

“Namjua vizuri Abuya, ni mchezaji aliyekamilika na kwa kweli ataisaidia sana Yanga kama wamemsajili. “Ni kiungo anayejituma anapokuwa uwanjani na anajua pia kufunga, na kwa jinsi ligi ya Bongo ilivyo, haiwezi kumsumbua kwa sababu amekomaa kiakili kama mchezaji.

 

“Nasema hivyo kwa sababu ameshacheza ligi ya Kenya miaka kadhaa, kwa hiyo ana uzoefu mkubwa kusema kweli kama Yanga wamesajili basi wamepata mchezaji mzuri,” alisema Santo na kuongeza:

 

“Hata Harrison Mwendwa ambaye pia anaichezea Kariobang Sharks anayedaiwa pia kujiunga na timu hiyo, pia ni mzuri akicheza nafasi ya kiungo mshambuliaji wa pembeni.

 

“Atawasaidia sana lakini katika nafasi ya kiungo Abuya yupo vizuri.” Hivi karibuni gazeti hili lilielezwa kuwa Zahera anatarajiwa kupewa fungu la usajili mapema kwa ajili ya msimu ujao kabla ya kuondoka kwenye majukumu ya timu ya taifa ya DR Congo, ambapo yeye ni kocha msaidizi wa taifa hilo na timu yake itashiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2019).

Comments are closed.