KUTOKA ‘SEBULENI ‘ HADI VIWANJANI

MAISHA yanakwenda kasi kweli! Wasanii wengi kwa sasa wanakimbizana na dijitali! Leo hii huyu anakimbiza kupata views kwenye Mtandao wa YouTube, yule kuuza nakala zake kwenye iTunes, Spotify na Tidal. 

 

Ukiangalia kwa undani utaona si kwenye kuuza nakala zao tu za audio au albamu, pia wapo bize katika kufunikana kwa rekodi mbalimbali katika shoo zao wanazotoa.

 

Mwishoni mwa Januari, mwaka huu, tumemuona staa wa muziki kutoka Nigeria, David Adeleke ‘Davido’ akiweka rekodi ya kuwa staa wa kwanza kutoka Nigeria na Afrika kwa ujumla kuuza tiketi zote 20,000 katika uwanja wa burudani wa 02 Arena pale London, Uingereza ambapo usiku huo alijaza ‘Wazungu’ wa kutosha!

 

Lakini kama hiyo haitoshi, staa wa komedi kutoka jijini Johannesburg, Afrika Kusini, Trevor Noah tayari ameweka oda ya kufanya bonge la tamasha katika ukumbi huohuo wa 02 Arena, Aprili 4, 2020 huku gumzo kubwa likiwa ni kwamba, ataipita rekodi ya Mwafrika mwenzake, Davido?

 

Tusubiri! Ukiachana na wakali hao wa Afrika, Kibongobongo dizaini kama ‘sumu’ hiyo ya kujaza viwanja imeanza kuingia. Wasanii wengi hususan wa Bongo Fleva wameanza kuhamia kufanya shoo za viwanjani.

 

Kweli tulipotoka ni mbali,  tunapokwenda ni karibu! Ikumbukwe kuwa miaka 5 nyuma, wakali wengi wa Kibongo kama wataenda kufanya shoo nje ya nchi basi tegemea shoo hiyo ni ya ‘sebuleni’ na kama ndani ya nchi watapiga shoo kubwa basi tegemea katika ukumbi f’lan tena unaojaza watu chini ya buku mbili tu, hiyo ndiyo Bongo ninayoifahamu!

 

Ikitokea wasanii wakafanya shoo kubwa basi tegemea kwanza hilo ni tamasha tena la msimu kama siyo Fiesta basi STR8 Muzik ambalo hukutanisha wasanii wengi kutoka ndani na nje ya nchi. Nadhani na wewe utakuwa umeifahamu Bongo hii kidogo!

 

Ninachotaka ujue, kwa sasa mambo yamebadilika Bongo, wasanii wanataka kufanya shoo za viwanjani ambapo wanaamini watawapata mashabiki wengi lakini pia itakuwa rekodi yao katika muziki. Katika makala haya, Showbiz Xtra limekuandalia baadhi tu ya wasanii ambao wapo katika maandalizi ya kudondosha shoo za uwanjani katika msimu huu wa sikukuu.

RAYVANNY

Ni msanii wa pili kusainiwa ndani ya Lebo ya Wasafi Classic Baby ‘WCB’ ambaye kwa sasa anafanya poa na Ngoma ya Tetema akiwa ameshirikiana na Diamond Platnumz.

 

Katika msimu huu wa sikukuu, Rayvanny atafanya shoo yake Idd Pili ndani ya Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live jijini Dar akisindikizwa na wakali kibao kama Juma Nature, Young Killer, Gigy Money na wengineo.

 

Katika usiku huo ulioitwa Vanny Day, Rayvanny anatarajia kuisimamisha Dar kwa muda wa saa kadhaa na foleni zote za daladala, bajaj, malori na gari ndogo kuelekea katika uwanja huo kupata burudani. Tusubiri tuone rekodi yake!

NANDY

Naweza kuthubutu kusema ndiyo msanii wa kike Bongo anayefanya poa kwenye Bongo Fleva kwa sasa akishindana na Vanessa Mdee ‘Vee Money’.

 

Licha ya kufanya huko poa, Nandy ambaye anapenda kujiita pia African Princess, anakuwa msanii wa kike wa kwanza kufanya shoo ya uwanjani ambapo katika Sikukuu ya Idd Mosi atakuwepo ndani ya Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga. Katika usiku huo tayari ameshaanza kuwaweka wakali watakaomsindikiza na miongoni mwao ni Billnass. Yajayo yanaweza kufurahisha sana!

 

DIAMOND

Ni staa wa Bongo Fleva mwenye kolabo nyingi nje ya nchi, naweza kusema kuliko msanii yeyote Bongo. Mara ya mwisho kwa Diamond kupiga shoo ya peke yake katika uwanja ilikuwa Dar Live, 2012 na alishuka kiwanjani hapo kwa helikopta na kuacha rekodi ambayo hadi leo hakuna msanii aliyewahi kuifunika. Safari hii, Diamond anatarajiwa kuweka rekodi nyingine kwa kufanya shoo ya peke yake katika Uwanja wa Kahama Idd Mosi na Geita Idd Pili.

 

Katika posti yake ya hivi karibuni, Diamond aliandika katika ukurasa wake wa Instagram; “Najiahidi mwenyewe mwaka huu nataka kuwapa hamasa vijana wenzangu kuwa na bidii, upendo, adabu na ukimuomba Mwenyezi Mungu kila kitu kinawezekana.

 

“Ndiyo sababu kuu ya shoo yangu hii ya KAHAMA na GEITA kuiita ONE MAN, ONE MIC …. yaani Uwanja wa KAHAMA na GEITA kama wanavyofanya wasanii wa Marekani basi nikaujaze mimi pekee DIAMOND PLATNUMZ tu na Mashabiki wa Muziki wa KAHAMA na GEITA…. !!!!! kwa nini wasanii wa nje waweze siye Tushindwe???” Rekodi hii nayo inasubiriwa!

HARMONIZE

Ni mkali mwingine kutoka WCB ambaye naye anatarajiwa kuujaza Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara katika Sikukuu ya Idd Mosi. Harmonize anatarajiwa kusindikizwa na wakali kibao kutoka ndani na nje ya nchi kama Skiibi na DJ Neptune kutoka Nigeria, Q Chillah, Country Boy na Queen Darleen kutoka Bongo. Napo ni rekodi nyingine ya kuisubiri!

 

MBOSSO

Anakuwa msanii wa nne kutoka WCB ambaye naye atafunga Uwanja wa Mkwakwani, Tanga katika siku ya Idd Pili. Katika usiku huu, Mbosso anatarajia kusimama peke yake kama ilivyo kwa bosi wake, Diamond. Swali ni je, ataweza kuweka rekodi, tusubiri!


Loading...

Toa comment