KWA HILI MLILOLIFANYA LULU DIVA, SANCHI MTASUBIRI TENA RAMADHANI 2020 ?

MWEZI Mtukufu wa Ramadhani ndiyo unaishia hivyo. Ulianza kama masihara masihara hivi, mara moja… mbili…tatu…, ile kushituka mwezi umegawanyika na sasa tunaelekea ukingoni. Wapo ambao wanasema bora uende maana umekuwa ukiwabana sana kufanya mambo yao, hasa baadhi ya mastaa.  Lakini niamini mimi, wapo ambao wanatamani uendelee kwa sababu ya faida ambazo wamezipata ndani ya Mwezi Mtukufu huu wa Ramadhani. Wanaotamani mwezi uishe haraka ni wale ambao kidogo wamemsahau Mungu. Wale ambao kutokana na mwezi walikuwa wakishindwa kufanya uzinzi, kunywa pombe

kuvaa mavazi ya ajabu ajabu na kufanya mambo mengine yasiyomfurahisha Mungu. Hawa ni watu wa ajabu sana! Lakini wapo ambao mwezi umewabadilisha. Mfumo wa maisha yao ya kila siku umebadilika, wamekuwa ni wachamungu, wanaojali masikini, wanaoheshimu kila mtu kiasi cha kutamani maisha yaendelee kuwa hivyo. Mbali na hilo, wapo ambao kufunga imekuwa ni kama kufanya dayati na miili yao imekaa sawa.

Katika hili mimi niseme tu kwamba, ndani ya mwezi huu kuna mambo mengi mazuri ambayo mastaa wameyaonesha. Hapa nawazungumzia mastaa waislam na wale wakristo. Kwa mfano, ndani ya mwezi huu kumekuwa na suala la kufuturisha. Baadhi ya wale ambao wamejaaliwa kufanya hivyo walifanya kwa staili walizojua.

Wapo waliofuata taratibu za kufuturisha lakini kuna wale ambao badala ya kufuturisha waliwalisha watu chakula cha jioni. Nikisema chakula cha jioni namaanisha kuwafuturisha watu wasiostahili, bila kufuata taratibu za kufuturisha na pia katika kufuturisha kwao wakawa wamemchefua Mungu. Hawa ni sawa na kwamba hawakufanya kitu. Mastaa ambao mwaka huu wamefurukuta kufuturisha, wapo wengi ila niwatolee mfano wawili ambao kwa walichokifanya natamani kifanywe na walio wengi tena bila kusubiri Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Hapa namzungumzia mwanamitindo Jane Ramoy ‘Sanchi’ na mwanamuziki Lulu Abbas ‘Lulu Diva’. Kwa nyakati tofauti mastaa hawa waliandaa futari kwa ajili ya watoto yatima. Lulu alifanya hivyo kwenye kituo cha kulelea watoto yatima kilichopo Magomeni Mikumi jijini Dar es Salaam kiitwacho Nabawiya Orphan Centre na Sanchi alikwenda kwenye kituo cha watoto yatima kilichopo Mbagala kiitwacho Alzam Orphan Centre.

Mastaa hawa wamefanya kitu kizuri ambacho kimeacha alama kwenye jamii. Hakuna asiyewajua mastaa hawa kwamba nje ya Mwezi Mtukufu wa wana tabia gani lakini kwa kuuheshimu wameamua kuweka pembeni kila kitu na kuamua kufanya yale ambayo Mungu ameridhia.

Kitendo cha wao kwenda kula futari na watoto yatima pamoja na kuwapa zawadi mbalimbali ni ishara ya upendo, kujali na kuthamini wengine. Na hicho ndicho ambacho tunatakiwa kukifanya kila wakati. Haiwezekani Mungu amekujaalia neema halafu unaitumbua bila kujali wale ambao wana uhitaji. Ukifanya hivyo ni lazima Mungu atafanya maamuzi ya kukurudisha kule ulikokuwa kwa kukupokonya neema aliyokupa.

Ndiyo maana kwenye makala haya nimependa kupongeza kile kilichofanywa na wadada hawa na naamini Mungu atawalipa kutokana na nia zao. Lakini sasa, kwa ninavyojua mimi ni kwamba, watoto yatima uhitaji wao hauwi ndani ya Mwezi Mtukufu tu. Kwamba wao watakuwa wanahitaji kula, kuvaa nguo nzuri, kulala sehemu salama na kupata matibabu ndani ya kipindi hiki tu.

Mambo hayo wanayahitaji katika kila siku ya maisha yao na kwa maana hiyo kama ni upendo wanastahili kuoneshwa kila siku. Hivyo basi, kama mastaa hawa watakuwa wamefanya haya mwezi huu tu kisha wakaingia mitini wakisubiri mwakani tena, jamii lazima itawashangaa.

Itawashangaa kwa sababu wao wamefika kwenye vituo hivyo, wamejionea hali halisi hivyo itakuwa ni jambo jema kama kwanza watashawishi na mastaa wengine kwenda kuwasaidia lakini ikibidi nao baada siku chache waende tena kuwaona na kuwasaidia kadiri Mungu atakavyokuwa amewaruzuku. Tukumbuke kwamba yatima na masikini wako kwenye himaya yetu hivyo tuna kila sababu ya kuhakikisha tunawapenda, tunawajali na kuwathamini. Tutambue kwamba furaha yao ni sisi, tukiwatenga ni lazima maisha yao yatakuwa magumu na watakosa hata lile tumaini la kuishi.

Shime aleikum ndugu zangu, mwezi umeisha na waliofanya mambo kwa ajili ya yatima na masikini ndani ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhani Mungu atawalipa lakini tusiishie hapo, tuendelee kufanya yale yaliyo ndani ya uwezo wetu kuhakikisha watu hao wanaishi kwa furaha. Tukumbuke kuwa alichotujaalia Mungu hakumaanisha tukitumie sisi na familia zetu tu bali ni ili na wengine wenye uhitaji nao wanufaike.


Loading...

Toa comment