The House of Favourite Newspapers

Kwa mazoezi haya ya Simba, kazi ipo

SIMBA! Simba! Itamke mara mbili kama ambavyo imechukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo. Hawa jamaa wanaonekana kweli wanautaka ubingwa mwingine wa tatu yaani hat trick.

 

Simba ambayo mpaka sasa ndiyo timu pekee iliyoshinda mechi zake zote nne za ligi kuu, ipo katika mazoezi makali kwelikweli kwenye Uwanja wa Gymkhana uliopo jijini Dar ikijiandaa na mechi zinazofuata. Mechi ya karibu zaidi ni ile dhidi ya Azam FC itakayopigwa Oktoba 23, mwaka huu kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar.

 

Azam FC wenyewe katika mechi mbili walizocheza wameshinda zote. Katika kuhakikisha wanautetea ubingwa wao, Simba chini ya Kocha Mbelgiji, Patrick Aussems imekuwa ikifanya mazoezi ya nguvu tangu Jumatatu iliyopita pale Gymkhana na wachezaji nao wanaonekana kuwa ‘siriaz’ kwelikweli.

 

Mazoezi ambayo Simba imefanya kwa siku mbili zilizopita ni ya kuwajengea stamina ili wachezaji wao wakikutana na mtu kama David Molinga ambaye ana mwili mkubwa wasitetereke.

Mazoezi ya juzi, wachezaji walitumia zaidi ya dakika 60, ambapo walikuwa wakikimbia huku wakivuta maparachuti kama Ulaya, wengine waliruka koni lakini baadhi wakivutana kwa kutumia kamba maalumu kwa ajili ya kuwajengea stamina katika miguu yao.

 

Jana uwanjani hapo, Simba ilifanya mazoezi ya kawaida ambayo yalianza saa 3 asubuhi ambapo wachezaji walianza kwa kukimbia mbio fupi na ndefu. Mbio ndefu walikimbia kwa raundi 12 sawa na fupi. Baada ya hapo walifanya mazoezi ya kunyoosha viungo wakiongozwa na Kocha wa Viungo, Adel Zrane raia wa Tunisia.

 

Akizungumzia mazoezi hayo, Aussems alisema kuwa, lengo kubwa ni kuwajengea wachezaji stamina ambayo itawafanya kuwa fiti tayari kwa mechi zijazo.

“Kwa sasa tunajiandaa na mechi zijazo za ligi, kama unavyojua hatutakuwa na mechi takribani wiki tatu kutokana na ratiba ya ligi kuu inavyoonyesha.

 

“Kwa hiyo kutokana na hali hiyo inatubidi kuhakikisha wachezaji wanaendelea kuwa fiti, ndiyo maana tumeamua kuwaandalia program kama hizi za mazoezi ili tutakaporudi uwanjani kazi yao iendelee kuwa juu,” alisema Aussems

Comments are closed.