The House of Favourite Newspapers

Lipuli FC wapewa Sh mil 15 waifunge Yanga

KATIKA kuongeza morali ya wachezaji ili wawafunge wapinzani wao Yanga, uongozi wa Lipuli FC umewaahidi wachezaji wao shilingi milioni 15 kama wakifanikiwa kuwafunga. Yanga na Lipuli zinatarajiwa kuvaana leo Jumatatu katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho utakaopigwa kwenye Uwanja wa Samora.

 

Katika mchezo huo, Lipuli wataingia uwanjani wakiwa na rekodi ya kuwafunga Yanga katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Samora, Iringa. Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, wachezaji hao wameahidiwa kupewa fedha hizo mara baada ya mchezo huo kumalizika kwa wao kushinda.

 

Mtoa taarifa huyo alisema, wachezaji wameahidi kupambana kufa au kupona kuhakikisha wanashinda mchezo huo unaotarajiwa kujaa upinzani mkubwa kutokana na maandalizi waliyoyapata kutoka kwa kocha wao, Selemani Matola.

“Tumeona umuhimu wa mchezo huu dhidi ya Yanga, hivyo ni lazima tushinde ili twende kucheza fainali na baadaye tuchukue kombe.
“Katika kuongeza hamasa ya wachezaji, tumeona tuwaahidi kiasi kidogo ambacho kwao kitakuwa kikubwa ili tufanikishe malengo yetu.

“Haitakuwa kazi nyepesi tunafahamu kwani Yanga nao wamepania mchezo huu kupata matokeo mazuri ya ushindi ambayo na sisi tunayahitaji,” alisema mtoa taarifa huyo.

Alipotafutwa Matola kuzungumzia hilo, alisema: “Bado sijazipata taarifa hizo rasmi, lakini hilo suala la ahadi linakuwepo mara kwa mara kwa viongozi wetu na uzuri ni kuwa wachezaji wangu wanajua umuhimu wa kila mechi.
“Kikubwa tunahitaji ushindi pekee katika mchezo wetu na Yanga, maandalizi yamekamilika na tunachosubiria ni mchezo huo.”

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Comments are closed.