The House of Favourite Newspapers

MADAI YA KUKUTWA NA MKE WA MTU CHUMBANI, ASKARI AKATWA NYETI

KUNA unyama ambao ukisimuliwa unaweza kusisimkwa na mwili; mfano ni huu wa mtu kuchukua kitu chenye ncha kali na kumkata mwenzake nyeti.

 

Tofautisha kuchanja na kukata yaani kuondoa sehemu ya kiungo kwenye eneo lake na kukitupa chini; ndivyo alivyofanyiwa askari mgambo aitwaye Sebastian ‘Seba’ mkazi wa Mtaa wa Majengo Kata ya Majengo, Halmashauri ya Mji wa Tunduma wilayani Momba mkoani Songwe.

 

KISA CHA KUKATWA NYETI NI HIKI

Vyanzo mbalimbali wakiwemo mashuhuda wa tukio hilo waliliamba Gazeti la Uwazi kuwa chanzo chake ni Seba kudaiwa kukutwa na mke wa mtu ambaye jina lake halikufahamika, anayeishi na mumewe Kijiji cha Chihanga, Wilaya ya Nakonde, nchi jirani ya Zambia. “Ijumaa iliyopita (Machi 15), nilimuona mwanamke huyo anaingia chumbani kwa Sebastian.

 

“Basi nikapuuza, lakini baada ya muda kuwa mwingi niliwaona wanaume watatu akiwemo mume wa  mwanamke huyo wanagonga kwenye chumba hicho na kudai kuwa wamemfumania. “Basi ndiyo wakamfanyia kitendo hicho cha kinyama cha kumkata nyeti kisha baadaye wakatoweka,” alisema Ester Mlungu, shuhuda wa tukio hilo.

ILIKUWAJE WAKAFUMANIWA?

Ilidaiwa na chanzo chetu kuwa Sebastian amekuwa na mazoea ya kwenda kununua mkaa kwa mke huyo wa mtu na kwamba siku ya tukio alidaiwa kutolipa fedha ya manunuzi ambapo alimtaka muuzaji (mke wa mtu) kwenda kuichukua nyumbani kwake.

MASWALI TATA

Kwa nini hakulipa na vipi amwambie mke wa mtu afuate fedha nyumbani kwake? Ni swali gumu, lakini ukweli unabaki kuwa mke huyo wa mtu alikwenda kwa Sebastian kuchukua fedha.

Ukiuliza kwa nini aingie mpaka chumbani wakati angeweza kuchukua fedha yake akiwa nje; mwenye jibu ni mke huyo wa mtu ambaye ametoweka pamoja na mumewe, lakini mashuhuda wanasema aliingia mpaka ndani. Hata hivyo, haikutosha kuingia tu, lakini inadaiwa muda aliokaa humo ndani ulikuwa mrefu ambao ndiyo unatajwa kuwapa viulizo wambeya ambao wanatajwa kumpasia maneno mume ambaye alitinga eneo la tukio akiwa na wapambe wake.

MTUHUMIWA AAMBIWA AJIPANGIE

Chanzo chetu kulilimbia Gazeti la Uwazi kuwa baada ya Sebastian kujikuta matatani, mwenye mke na wapambe wake walimwambia achague adhabu. “Walipomwambia achague adhabu akabaki kuwaomba msamaha, walipoona anashindwa kuchagua, wakaamua kumkata nyeti,” kilidai chanzo.

KWA NINI NYETI NA SIYO MGUU

Pengine angeambia kukatwa nyeti na mguu achague moja angeweza kuchagua mguu, lakini hakupewa nafasi hiyo na kwamba mafisadi hao waliamua kumchagulia cha kumkata.

WATUHUMIWA WATOWEKA

Ingawa inatajwa kuwa yalikuwa ni majira ya saa tisa alasiri, lakini Sebastian wakati anafanyiwa kitendo hicho chenye maumivu makali hakupiga kilele hadi watuhumiwa walipotoweka kusikojulikana ndipo alipoomba msaada kwa wasamaria wema. Chuki Kibaya, mkazi wa Tunduma, alisema walimkuta Sebastian akilia huku akiwa ameshikilia nyeti yake walipomuuliza ndipo alipowapa mkasa wa kuvamiwa na watu hao raia wa Zambia na kufanyiwa ukatili huo.

KAKA WA SEBASTIAN ANENA

Lackson Mwazembe ni kaka wa mtuhumiwa huyo, yeye alisema baada ya kupata taarifa ya mdogo wake kukatwa nyeti alikwenda kumchukua na kumpeleka Polisi. “Tulipofika Polisi tulitoa taarifa na baadaye kupatiwa fomu namba tatu ‘PF-3’ kwa ajili ya matibabu kisha tukampeleka hospitalini kupatiwa matibabu katika Kituo cha Afya cha Tunduma.

AFISA MTENDAJI WANENA

Rashid Enock, Afisa Mtendaji Mtaa wa Majengo B, alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kusema kuwa alifika kujionea kitendo hicho cha kinyama. “Nilikwenda huko na kumuona majeruhi, baadaye nilishirikiana na kaka’ke kumpeleka Polisi kisha hospitalini,” alisema.

MWENYEKITI WA MTAA AFUNGUKA

Kajambo Mwampanja, Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo B, alisema baada ya kufika eneo la tukio na kujionea hali halisi, aliitisha mkutano wa dharura na kuwaonya wananchi kuacha tabia hiyo ya kujichukulia sheria mkononi kwa vile nchi yetu inaogonzwa kwa misingi ya sheria.

“Hadi sasa taratibu za kuwasiliana na Serikali ya Wilaya ya Nakonde kuwapata watuhumiwa zinafanyika licha ya kuwa bado majina yao hayajafahamika. “lla viongozi wangu wa wilaya tayari nimewasiliana nao na wameniambia kuwa wanalishughulikia sakata hili,” alisema.

HUYU HAPA MKUU WA WILAYA

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani Momba ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo, Juma Irando, licha ya kukiri kupokea taarifa ya tukio hilo pia alisema amewasiliana na mkuu wa Polisi ili hatua zichukuliwe.

MSIKIE DAKTARI

Akizungumzia uwezekano wa majeruhi huyo wa kuunganishwa nyeti yake kitaalam na uwezekano wa kurudia hali yake ya zamani dokta maarufu jijini Dar, Richard Marise alisema:

“Inategemea na muda aliofika hospitalini, kama aliwahi uwezekano wa kuunganisha upo, lakini kurudia hali yake kama zamani ni jambo gumu kidogo.” Majibu hayo yanamuweka katika hali ngumu Sebastian ya kupona na kurejea hali yake ya zamani na kwamba huwenda akawa amepewa kilema cha maisha.

Stori: IBRAHIM YASSIN, TUNDUMA

Comments are closed.