MWAKA 1978 jeshi letu lilipigana vita na Nduli Iddi Amini wa Uganda na lilikuwa na mameja jenerali wawili tu, Meja Jenerali Abdallah Twalipo aliyekuwa mkuu wa majeshi wakati huo na Meja Jenerali Mirisho Sarakikya.
Pia lilikuwa na mabrigadia saba tu: Brigadia Mwita Marwa, Brigadia David Musuguri, Brigadia Silus Mayunga (Mti Mkavu), Brigadia John Walden (Black Mamba), Brigadia Tumainia Kiwelu, Brigadia Yusuf Himid na Brigadia Nelson Mkisi. Chini ya mabrigadia kulikuwa na makanali kadhaa akiwemo Moses Nnauye, Abdallah Natepe na wengineo.
Jeshi letu lilikuwa limegawanyika katika brigade nne: Kusini, Magharibi, Mashariki, na Zanzibar. Baada ya vita ya Kagera ndipo Twalipo alipopandishwa cheo na kuwa Luteni Jenerali na mabrigadia walipandishwa kuwa ma-meja jenerali.
Muundo wa jeshi letu ukabadilishwa kidogo kuwa na division tatu. Miaka miwili baadaye Luteni Jenerali Twalipo alipandishwa cheo tena na kuwa Jenerali kamali.
Baadaye sana cheo cha Brigadia kilibadilishwa na kuwa Brigadia Jenerali.
Wakati wa vita ya Kagera makamanda walikuwa na majina bandia kama vile Black Mamba, Mti Mkavu, Kambare; majina hayo yalikuwa maalumu ili kuficha utambulisho wao halisi hasa kwenye mawasiliano ya kijeshi vitani.
Mfano Meja Jenerali Mwita Marwa aliitwa Kambale kwa sababu yeye na brigade yake walipigana vita ya Kagera wakiwa ndani ya maji kwa muda wa wiki mbili, maji yanayofika kiunoni na bado walijitoa kimasomaso kukabiliana na adui.
Makamanda walioongoza vita ya Kagera walikuwa wengi ni pamoja na Brigadia Marwa, Brigadia Mayunga, Brigadia Kiwelu, Brigadia Kimario na Brigadia Walden (Black Mamba). Hawa ndio walioingia msituni na wapiganaji.
Makamanda hawa walipata vyeo vyao hivyo kutokana na umahiri wao katika uongozi wa kijeshi, na wote walihudhuria mafunzo ya uongozi wa kijeshi ndani na nje ya nchi mara kadhaa.
Brigadia Moses Nnauye (baba yake Nape Nnauye) alishiriki kama muhamasishaji. Anatajwa kuwa alikuwa anaweza kuwahamasisha askari mpaka wengine walisahau kama kuna kufa vitani na alikuwa na uwezo mzuri sana wa kujieleza na kumwelezea adui alivyo dhaifu mpaka askari kumuamini kuwa kweli adui si chochote, atafumuliwa.
Katika makamanda waliopiganisha vita kitaalamu na kwa ufundi wa hali ya juu, anatajwa pia Jenerali Amran Kombe.
Jenerali Msuguri anatajwa kuwa hakuwa msomi lakini mabrigedia wake walikuwa wana elimu ya kutosha na ndiyo maana waliweza kupanga mashambulizi ya kiufundi dhidi ya Iddi Amini wa Uganda.
Luteni Kanali Ben Msuya anatajwa kuwa aliongoza utekaji wa jiji la Kampala, na akawa Meya wa Jiji hilo kwa muda, mkuu wa itifaki, na mwisho kuandaa shughuli ya kuapishwa Rais Profesa Yussuf Lule.
Luteni Kanali Hassani Boma na Luteni Kanali Mazora wametajwa kwa umahiri wao katika medani ya vita.
Meja Jenerali Silas Mayunga “Mti Mkavu” ndiye aliingia kijiji cha Koboko ambako alizaliwa Iddi Amini. Baada ya Mbarara kutekwa, Mayunga alipandishwa cheo kuwa Meja Jenerali na kupewa Brigade mbili kuziongoza.
Chini yake walikuwepo Brigadia Hemedi Kitete na Brigadia Roland Makunda. Pia walikuwepo Brigadia Jenerali Ramadhani Haji Faki, mmoja wa makamanda kutoka Zanzibar.
Tangu tupate uhuru, wakuu wa majeshi na miaka yao katika mabano walikuwa kama ifuatavyo: Mirisho Sarakikya (1964-1974), Abdallah Twalipo (1974-1980), David Musuguri (1980-1988), Ernest Mwita Kiaro (1988-1994), Robert Mboma (1994-2001), George Waitara (2001- 2007), David Mwamunyange (2007- 2017), na sasa Venance S. Mabeyo.
Kifupi ni kwamba, tunajivunia jeshi letu ambalo wakati wa amani husaidia shughuli mbalimbali za kijamii.