
KUTOKANA na kukithiri vitendo vya rushwa nchini Kenya, Kiongozi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Noordin Haji amemuagiza Ispekta Mkuu wa polisi nchini humo, Hillary Mutyambai kuangalia uwezekano wa kuwafunga kamera za CCTV mwilini mwao askari wa usalama barabarani ili kukabiliana na vitendo hivyo.
Hatua hiyo imekuja baada ya kukithiri kwa makosa ya kujaza abiria kupita kiasi katika mabasi na daladala nchini humo huku trafki wakikaa kimya bila kuwachukulia hatua dereva na wamiliki wa gari hizo.
“Kuhakikisha sheria zinafuatwa barabarani, kupunguza polisi kutumia mamlaka yao vibaya, kusaidia watu wasivunje sheria na kuwezesha uchunguzi na kupunguza ufisadi, ni muhimu kufikiria jinsi unaweza kuhakikisha maafisa wa trafiki wana kamera mwilini,” alisema Haji.
Katika barua kwa Mutyambai, Haji anasema itakuwa vigumu kujua iwapo abiria alikataa kutii aliyoambia kuwa gari limejaa au lah!.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari nchini humo, Mkuu wa polisi Hillary Mutyambai alitoa amri abiria wote wanaozidi kwenye gari wakamatwe.
“Kulingana na maoni yangu, itakuwa vigumu kupata ushahidi wa kutosha kuonyesha abiria wa ziada walikataa kusikiliza amri ya afisa wa polisi, au walikataa kuwasikiliza utingo au dereva kuwa wasiingie kwenye gari,” alisema haji
Kulingana na sheria hizo za trafiki ndio wanaweza kuwapiga faini, utingo, dereva na mmiliki wa gari kuanzia Sh 113,000 kwa kiwango cha chini hadi na Sh milioni 4.5 kwa kiwango cha juu.
Stori: Mwandishi Wetu na Mitandao