Makambo aaga Yanga, afunguka

MSHAMBULIAJI wa Yanga Mkongomani, Heritier Makambo amewashukuru mashabiki wa timu hiyo kwa sapoti waliyompa katika kipindi cha mwaka mmoja ambacho ameitumikia klabu hiyo.

 

Hiyo, ikiwa ni siku chache tangu asafiri kwenda nchini Guinea kwa ajili ya kufanya vipimo Klabu ya Horoya AC iliyoonyesha nia ya kumsajili kwa ajili ya kumtumia kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika watakayoshiriki.

 

Makambo yupo katika hatua za mwisho kwa ajili ya kukamilisha uhamisho wa kwenda kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Guinea ambao ni Horoya AC iliyopanga kukiimarisha kikosi chake.

 

Mshambuliaji huyo mwenye mabao 16 katika msimu huu wa ligi, aliwaaga mashabiki wa Yanga kupitia moja ya akaunti yake ya mtandao wa kijamii na kuandika hivi:

“Nitawakumbuka mashabiki wa Yanga kwa upendo na sapoti yao kwangu. Watabaki moyoni mwangu,” aliandika Makambo.

 

Mshambuliaji huyo alitua Yanga kutoka FC Lupopo ya DR Congo kwa mkataba wa miaka miwili, atakuwa ametumikia nusu ya mkataba wake, hivyo kuinufaisha Yanga katika mauzo yake.

 

Aidha, Mkurugenzi wa Ufundi wa Horoya AC anatarajiwa kutua nchini Tanzania wiki hii kwa ajili ya kufanya mazungumzo na viongozi wa Yanga ili kukamilisha dili hilo la usajili.

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam


Loading...

Toa comment