The House of Favourite Newspapers

MAPYA YAIBUKA ALIYEPIGWA RISASI NA MWANAJESHI

PWANI: TUKIO la kijana Juma Mbwate (26) mkazi wa Mwananyamala Kisiwani, Dar, ambaye wiki moja iliyopita aliuawa kwa risasi na wanajeshi waliokuwa lindoni maeneo ya Mapinga, Bagamoyo Mkoa wa Pwani limeibua mapya, Uwazi linakupa habari kamili. 

 

Akizungumza kwa uchungu kaka wa marehemu Ramadhani Mohamed ambaye ndiye alikuwa akiishi naye aliibua mapya kwa kueleza kwamba mdogo wake alikuwa na matatizo ya akili ya kuzaliwa nayo.

 

Pamoja na matatizo hayo pia tatizo lingine ni kuwa mara nyingi zikifika nyakati za usiku macho yake yalikuwa hayaoni mbali. Aliendelea kusema kuwa alikuwa akikaa na marehemu kwa wiki moja na wiki nyingine akawa anaenda Bagamoyo kwa ndugu zake wengine kwa hiyo alikuwa akiishi sehemu mbili.

 

Ramadhani aliendelea kueleza kuwa siku ya tukio mdogo wao aliondoka nyumbani Mwananyamala bila wao kujua na kwenda Bagamoyo lakini alipigiwa simu na rafiki yake mmoja na kumwambia kuwa jana yake usiku alimuona Juma amekatiza sehemu yeye akiwa amekaa sehemu akiwa anakunywa soda. Rafiki huyo alimweleza kuwa baada ya siku hiyo kupita kesho yake wakatangaziwa kuna mtu amepigwa risasi na wanajeshi alikuwa akiparamia ukuta wa jeshi hivyo mwenye ndugu yake kapotea aende Kituo cha Polisi Mapinga.

 

“Unajua mara nyingi ndugu yangu akiondoka kwenda Bagamoyo lazima tupeane taarifa ndugu wa huku na kule kutokana na matatizo aliyonayo lakini siku hiyo haikuwa hivyo mpaka rafiki yangu aliponiambia ana wasiwasi anayetangazwa anaweza kuwa ni Juma maana alimuona usiku akielekea huko kambini hivyo tufanye uchunguzi.

 

“Baada ya kupewa taarifa hizo na rafiki yangu niliwapigia simu watu wa nyumbani Bagamoyo na kuwauliza kama wamemuona Juma, wakasema hawajamuona hivyo wakapeana majukumu wengine wakaenda Mochwari Bagamoyo na wengine Kituo cha Polisi Mapinga,”alisema.

 

Alieleza kuwa baada ya kila mmoja kwenda alikopangwa walikuta kweli ni yeye lakini pale polisi walikuta changamoto kuwa kuna mama alikuja alidai huyo ni mumewe na wamezaa naye watoto kitu ambacho hakiwezekana kwani ndugu yao huyo hajawahi kuzaa wala kuwa na mke wala mwanamke yeyote maishani mwake kutokana na matatizo ya akili aliyokuwa nayo.

 

“Tulijaribu kuwaambia polisi kuwa ndugu yetu alikuwa ni mgonjwa wa akili na tuliwaonyesha vyeti vyake vyote na kuwaambia kuwa hajawahi kuzaa kutokana na matatizo yake lakini tuliambiwa kuna mwanamke amekuja na yeye anadai ni mume wake na amezaa naye watoto hivyo tusubiri,” alisema kaka huyo.

 

Hata hivyo, alisema kuwa kila siku wamekuwa wakifuatilia mwili wa ndugu yao ili wakamzike bila mafanikio kwani wanaambiwa mpaka vipimo vya vinasaba vya watoto wa yule mama aliyedai ni mumewe vije ndiyo wanaweza kufanya lolote.“Nimejaribu kuwatajia kila kovu lililopo mwilini kwa mdogo wangu kwa sababu namjua vizuri lakini wapi na inaumiza kifo alichokufa kwani alikuwa hafahamu lolote lile kwa kuwa alikuwa mgonjwa wa akili.

 

“Hatujui tutapewa lini mwili wa ndugu yetu kwa sababu mpaka sasa ni siku ya kumi,” alisema. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, ACP Wankyo Nyigesa alipopigiwa simu na kuulizwa kisa cha ndugu kutopewa mwili wa marehemu ili wakauzike alisema kuna matatizo ambayo hangeweza kusema kwa wakati huo kwa sababu alikuwa sehemu mbaya.

 

“Nitakujulisha nini sababu, hapa nilipo siyo sehemu nzuri, nitakupigia baadaye kukujulisha kwani sababu zipo,” alisema Kamanda Nyigesa. Hata hivyo hadi tunakwenda mitamboni hakupiga simu chumba chetu cha habari kama alivyoahidi.

STORI: IMELDA MTEMA, UWAZI

Comments are closed.