Mashine Nyingine Nne Zatua Dar kusaini Yanga

HII ni kufuru! Hivyo ndivyo utakavyoweza kusema kwa Yanga ambayo juzi usiku ilishusha mastaa wanne kwa ajili ya kusaini mkataba wa kuichezea timu hiyo na kati ya hao yupo mshambuliaji wa Zesco ya Zambia, Maybin Kalengo aliyetarajiwa kumwaga wino jana usiku.

 

Yanga hivi sasa ipo kwenye mipango ya kukisuka kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao kwa kuhakikisha inasajili wachezaji watakayoirejesha anga za kimataifa. Timu hiyo, tayari hadi hivi sasa imekamilisha usajili wa wachezaji watano kati ya hao ni viungo washambuliaji, Patrick Sibomana (Mukura FC), Issa Bigirimana (APR) na beki wa kushoto, Erick Rutanga anayeichezea (Rayon Sports) na beki Mghana, Lamine Moro.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa, timu hiyo juzi usiku ilimshusha kiungo mkabaji, Mohammed Mushimiyimana maarufu kwa jina la Meddie anayeichezea Police FC ya Rwanda.

 

Mtoa taarifa huyo alisema, pia timu hiyo imempokea Kalengo ambaye ni kati ya washambuliaji tegemeo hivi sasa wanaoichezea Zesco ya Zambia ambaye naye ametua nchini juzi usiku kwa ajili ya kufanya mazungumzo na kusaini mkataba.

 

Aidha, mtoa taarifa alisema kuwa, Yanga imefanikisha usajili wa kiungo mkabaji wa Mafunzo FC ya Visiwani Zanzibar, Abdul Aziz Makame ambaye naye amesaini mkataba wa miaka
miwili.

 

“Usajili wetu unakwenda vizuri na bado tunaendelea kufanyia kazi ripoti ya kocha (Mwinyi) Zahera ambayo ameitoa kwa uongozi ambao unaendelea kufanya usajili kwa mujibu wa ripoti yake aliyoiacha kwa uongozi.

 

“Juzi (jana) usiku tulipokea wachezaji wawili kutoka nje ya nchi ambao wamekuja kwa ajili ya kukamilisha usajili wao ambao ni kiungo kutoka Police FC ya Rwanda ambaye ni Mushiyimana maarufu kwa jina la Meddie.

 

“Meddie anacheza nafasi ya kiungo mkabaji namba sita, pia ana uwezo wa kucheza namba nane na amekuja kwa ajili ya kufanya mazungumzo kabla ya kusaini mkataba wa miaka miwili ya kuichezea Yanga.

 

“Pia, tumempokea mshambuliaji mmoja mwenye kasi na nguvu ya kupambana na beki yeyote ambaye ni Kalengo yeye anatokea Zesco ya Zambia na kama mipango itaenda sawa basi atasaini mkataba wa miaka miwili Yanga,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela kuzungumzia hilo alisema: “Tayari tumekamilisha usajili wa wachezaji watano ambao tayari wamesaini mikataba kati ya hao yupo mmoja mzawa ambaye ni Makame lakini wengine wote ni kutoka nje ya nchi.

 

“Waliotoka nje ya nchi ambao wamesaini mikataba ni Sibomana, Bigirimana, Rutanga na Lamine pekee, lakini uongozi unaendelea kuwapokea wachezaji wengine kutoka nje ya nchi wanaofika kwa ajili ya kusaini mikataba tuliopanga kuwatangaza rasmi baada ya kukamilisha dili.”

Loading...

Toa comment