The House of Favourite Newspapers

Mastaa Mnaijua Thamani ya Imani za Dini Zenu?

Staa wa Bongo, Irene Uwoya.

WENGI wetu tulipozaliwa, tuliwakuta wazazi wetu wakiwa na dini zao. Tulichokifanya sisi ni kufuata imani zao. Leo hii ukiniuliza kwa nini ni Muislam, nitakuambia ni kwa sababu wazazi wangu ni Waislam.

 

Kinachofanyika ni kwamba, mtoto akizaliwa, akishafikisha umri wa kuelewa mambo, anaanza kuelezwa kuhusu imani ya wazazi wake na baadaye kupelekwa kwenye mafundisho rasmi. Kama ni Mkristo atapelekwa kanisani na kama ni Muislam atapelekwa madrasa. Taratibu imani inaanza kumuingia na inafika kipindi anakuwa ameiva katika dini yake.

 

Mtoto akishaijua vizuri dini, akawa na imani nayo ni ngumu sana kumhamisha. Atabaki kwenye imani yake mpaka pale ambapo

Mungu atamchukua. Kubadili dini kwa mtoto huwa ni jambo la nadra sana licha ya kwamba anapofikisha umri flani ana uhuru wa kuamua.

 

Jacqueline Wolper

Ndiyo maana mara kadhaa tumekuwa tukishuhudia baadhi ya watu kwa sababu mbalimbali wakizihama dini zao na kuhamia nyingine. Jambo hili mara nyingi haliwaridhishi wazazi lakini wengi wanafikia hatua ya kukubaliana na uamuzi wa watoto wao kwa kuwa wameshakuwa wakubwa.

 

Katika hili la kubadili dini, baadhi wamekuwa wakilifanya na mara nyingi hufikia hatua hiyo pale wanapotaka kuingia kwenye ndoa. Unakuta mwanaume ambaye ni Muislam anatokea kumpenda binti ambaye ni Mkristo. Katika makubaliano yao mmoja wao analazimika kubadili dini kumfuata mwenzake.

 

Hilo wala sina shida nalo kwa sababu wanaofanya hivyo ni watu na akili zao. Tatizo ni pale ambapo unakuta mtu anaamua kubadili dini kwa sababu ya kumfuata mpenzi wake ili waoane lakini wala haoneshi kwamba amebadili dini.

 

Yaani yupoyupo tu. Kama alikuwa Mkristo na kuingia Uislam, utamuona anajifanya kuvaa mabaibui lakini huwezi kumuona anaingia msikitini hata siku moja. Sasa unabaki kujiuliza kwamba, huyu atakuwa kabadili dini kweli au kazuga tu ili aolewe?

 

Hili lipo sana kwa mastaa wetu wa Bongo. Kwenye kumbukumbu zangu kuna mastaa zaidi ya watano ambao waliwahi kutangaza kubadili dini. Wote hao walifanya hivyo kwa sababu za kimapenzi.

 

Zaidi ya mara mbili msanii wa filamu Bongo, Jaqueline Wolper aliwahi kubadili dini na kuwa Muislam kwa kuwafuata wanaume. Sikuwahi kuona dhahiri kwamba alibadili dini, niliona kama amefanya sanaa tu, mwisho akarudi kwenye dini yake ya Ukristo.

 

Achana huyo, Irene Uwoya naye siku za hivi karibuni alibadili dini na kuwa Muislam huku akijipa jina la Sheila. Alifanya hivyo kwa madai ya kwamba ni ili aolewe na msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Abdulaziz Chende ‘Dogo Janja’.

 

Naye sikuwahi kuona kama kweli alikuwa Muislam. Alibaki Uwoya yuleyule na hata ndoa yenyewe haikufika mbali ikavunjika. Leo hii anaulizwa kama amerudi kwenye dini yake anadai hakuwahi kubadili dini. Huku si ni kuleta usanii kwenye mambo ya msingi jamani? Hivi unawezaje kutangaza kwamba umesilimu halafu baadaye inabainika siyo kweli? Huku ni kumtania Mungu.

 

Lakini katika hili nichukue nafasi hii kuwapongeza wanamuziki Khadja Maige ‘Khadija Nito’, Hafsa Kazinja, Flora Mvungi na Charles Gabriel ‘Chaz Baba’ ambao walipotangaza kwamba

wamebadili dini, walimaanisha.

Hafsa na Khadja wametoka kwenye Uislam na kuingia kwenye Ukristo na wanaonekana walikuwa siriasi kwenye uamuzi huo. Katika kuwafuatilia nimebaini wadada hawa kweli wamempokea Yesu na wanaishi katika ile misingi inayokubalika.

 

Hata mwanadada Flora Mvungi ambaye alitoka kwenye dini yake ya Kikristo na kuingia kwenye Uislam kisha kuolewa na mwanamuziki Hamis Baba ‘H-Baba’, alionesha kuwa kweli amebadilika na aliwahi kuonekana akiingia msikitini.

Aidha, msanii wa muziki wa dansi, Chaz Baba naye hivi karibuni alidhihirisha kuwa, siyo mastaa wa kike tu wanaobadili dini kwa sababu ya ndoa bali hata wanaume.

Yeye alitoka kwenye Ukristo na kuingia kwenye Uislam kisha kufunga ndoa na mwanadada aliyefahamika kwa jina la Mariam.

 

Ndiyo maana mwanzo nikasema kuwa, siyo jambo baya mtu kubadili dini lakini shida inakuja pale ambapo unabadili dini kisha unaonekana kama bado uko kwenye dini yako ya awali. Lakini pia kitendo cha leo umebadili dini kisha kesho ukarudi kwenye dini yako ya mwanzo, huko ni kumtania Mungu na hiyo inaonesha kuwa, hauko makini na maisha yako.

Tukumbuke kwamba suala la imani si la kuletea usanii, ukiamua kuifuata dini flani, ifuate kikwelikweli. Hii ni kwa sababu, ukiwa huna imani iliyo thabiti, maisha yako lazima yatayumba. Hivyo nashauri kila mmoja aiheshimu imani yake na kutokubali kuyumbishwa na walimwengu.

STORI NA NA AMRAN KAIMA | UWAZI

Comments are closed.