The House of Favourite Newspapers

Matatizo Katika Ute wa Uzazi kwa Mwanamke

0

NA DK. CHALE | IJUMAA | AFYA

MATATIZO katika ute wa uzazi wa mwanamke kitaalamu tunaita Abnormal Cervical Mucus . Ute wa uzazi anaoupata mwanamke pale anapokuwa katika kipindi cha upevushaji mayai ndiyo unaosaidia mbegu za kiume ziweze kusafiri hadi katika yai lililopevuka katika mrija wa uzazi. Kwa kawaida ute wa uzazi ni mwepesi na unavutika au unakuwa na mnato.

Matatizo ya uzazi yanayomfanya mwanamke asipate ujauzito husababishwa na kasoro katika uzalishaji wa mbegu za kiume na matatizo katika ute wa uzazi. Tunategemea mwanamke yeyote aliye kamili katika uzazi hupevusha mayai na dalili ya upevushaji huu wa mayai ni kuwa anatokwa na ute wa uzazi.

JINSI TATIZO LINAVYOTOKEA

Kupata ute wa uzazi usio wa kawaida kwa mwanamke humfanya awe mgumba, ute wa uzazi unapokuwa na tatizo husababisha mbegu za kiume zishindwe kupenya humo na kuogelea kwenda kurutubisha yai lililo tayari. Pia ute wenye matatizo huua au kuziharibu mbegu za kiume, hata mwanaume atoe mbegu zenye ubora namna gani kama pale ukeni ute una matatizo basi zitauawa au kukosa ubora wa kwenda mbele zaidi.

Tunapoongelea ute wa uzazi kwa kawaida ute huu tunauweka katika makundi makuu matatu, kwanza ni ute mzito, ute huu baada ya muda mfupi hubadilika kuwa mwepesi na mwembamba huku ukivutika kwa lengo la kuwezesha mbegu za kiume zisafiri humo, mwisho ute wa uzazi unarudi kuwa mzito.

Ute wa uzazi unapokuwa mwepesi na kuvutika unaashiria uwepo wa kiwango cha kutosha cha vichocheo vya Estradiol katika mzunguko mzima wa mfumo wa hedhi wa mwanamke. Hapa tunategemea vichocheo hivi vya Estradiol kuwa vizuri hasa katika kipindi cha uzalishaji mayai kiitwacho Follicular Phase .

Mwanamke mwenye ute wa uzazi usio wa kawaida yaani anakuwa na ute mzito tu daima, hana historia ya kupata ute mwepesi na wa kuvutika tunasema anapevusha mayai lakini hatoi ute wa uzazi hivyo kuna matatizo katika utoaji wa ute wa uzazi tatizo ambalo kitaalamu linaitwa Abnormal Cervical Mucus.

Kwa hiyo mwanamke anaweza kuwa na tatizo hili la kutokupata ute wa uzazi wenye sifa katika kipindi chote cha umri wake wa kuzaa na hata wakati wa Ovulation au upevushaji wa mayai. Ute huu mzito ukeni husababisha kuua au kuziharibu mbegu za kiume na wakati mwingine hutoa nafasi kwa bakteria na fangasi kujipenyeza humo na kumfanya mwanamke asumbuliwe na tatizao la muwasho wa mara kwa mara ukeni, kutoa harufu mbaya au ute huo kubadilika rangi na kuwa njano.

Tatizo linaweza kuendelea na kuathiri mlango wa kizazi hivyo mwanamke anapata ugonjwa uitwao Cervicitis. Wakati mwingine ute huu usio wa kawaida unaweza kutengeneza mazingira ya kinga ukeni ambapo kila mbegu ya kiume inapofika ukeni inauawa.

Ute huu ukigunduliwa mwanamke hutibiwa na kupona na kupata ujauzito, itakuwa ngumu endapo mwanamke huyu atakuwa na maambukizi sugu ukeni au mdomo wa kizazi utabana kutokana na matibabu ya saratani ya shingo ya kizazi.

UCHUNGUZI

Uchunguzi wa tatizo hili hufanyika katika kliniki za madaktari bingwa wa akina mama kwenye hospitali za mkoa ambapo vipimo vya kuangalia ute wa uzazi na shingo ya kizazi vitafanyika. Vilevile vipimo vya mbegu za kiume vitafanyika kuangalia ubovu wa mbegu na kama kweli zinashindwa kupenya na kuogelea katika ute wa uzazi. Vipimo vingine ni damu kuangalia homoni za uzazi na vingine ambavyo daktari ataona vinafaa.

TIBA NA USHAURI

Matibabu hutolewa baada ya uchunguzi wa kina, endapo mume na mke wana tatizo la kutopata mtoto kwa mwaka zaidi ya mmoja, basi uchunguzi ufanyike kwa wote wawili. Baada ya uchunguzi wa ute kwa mwanamke kukamilika, tiba hutolewa kwa kukabili tatizo na kulainisha uke ili mbegu za kiume ziwe na uwezo wa kulifikia yai. Matibabu mengine yatatolewa kadiri daktari atakavyoona inafaa.

Leave A Reply