
Uwanja wa Masjid Quba, Sinza, uligeuka uwanja wa vita jioni hii, waendesha bodaboda wanaoshabikia Simba na Yanga wakimenyana kwenye Sinza Bodaboda Cup. Mashabiki walijazana kushuhudia kandanda la vumbi lenye tambo, chenga za maudhi, na mashuti makali – lakini bao likawa bidhaa adimu.
Licha ya juhudi za kila upande, mabeki na makipa walidumu imara, na dakika 90 zikamalizika kwa sare tasa ya 0-0.
Mchuano huu wa kukata na shoka ulivuta hisia si tu kwa mashabiki wa uwanjani, bali pia kwa watazamaji waliokuwa wakifuatilia mubashara kupitia Global Online TV. Kelele za tambo na shangwe kutoka Sinza zilisikika mitandaoni, huku mashabiki wakichangia mijadala motomoto kuhusu ubora wa vikosi na maamuzi ya waamuzi.
