Maumivu chini ya kitovu kwa wanawake!

MAUMIVU chini ya kitovu kwa wanawake kitaalamu huitwa Lower Abdominal Pain, ni tatizo ambalo huwakumba hata wanaume lakini kwa bahati mbaya wengi hulichukulia kuwa ni jambo la kawaida kitu ambacho baadaye husababisha wagonjwa kuingia kwenye matatizo makubwa ya kiafya hasa kwenye mfumo wa uzazi na mfumo wa chakula. Maumivu chini ya kitovu yapo yale ya chini yake, katikati, kushoto na kulia.

MAUMIVU KWA WANAWAKE

Kwa wanawake maumivu ya kushoto na kulia yapo ya aina mbili. Kuna yale ambayo yanakuwa upande mmoja lakini husambaa kwa urefu wa sentimita mpaka nne na inaweza ikawa upande mmoja au pande zote mbili lakini yapo mengine chini ya kitovu ambayo yanaweza yakawa upande mmoja au pande zote mbili bila kusambaa kwa marefu.

Kuna maumivu mengine chini ya kitovu huwapata wanawake wakati tu wanaposhiriki tendo la ndoa kwa ndani ya uke au chini ya kitovu. Pia yapo ambayo huwapata wanawake wakati wameinama, wakati wa kunyanyua vitu vizito, wakati wa kucheka au kuimba na wakati mwingine wakiwa wamelala kifudifudi.

Maumivu chini ya kitovu yanaashiria matatizo kwa wanawake kama vile mirija ya uzazi kujaa maji mazito na machafu ambayo huzuia yai kutembea kwenye mirija ya uzazi.

Mwanamke ambaye amewahi kuambiwa na daktari kwamba anatakiwa asafishwe kizazi chake au mirija ya uzazi na wakati huo huo anasikia maumivu chini ya kitovu kushoto na kulia au upande mmoja, kuna uwezekano akawa na tatizo la mirija ya uzazi kuziba kutokana na kujaa maji machafu.

Lakini pia maumivu hayo yanaashiria kutokukomaa kwa mayai ya uzazi. Hii husababisha vifuko vya mayai ya uzazi (Ovaritis) kuvimba na kumletea mwanamke maumivu chini ya kitovu mithili ya kichomi.

Mwanamke ambaye ana maumivu chini ya kitovu na wakati huo huo ana matatizo ya hedhi kukoma au kutokuwa na mpangilio maalum kuna uwezekano mkubwa akawa na tatizo la vifuko vyake vya mayai ya uzazi kutokomaza mayai na hivyo mayai kutotoka kwenye vifuko hivyo na kusababisha kuvimba na hatimaye kumsababishia mwanamke maumivu makali au kitu kama kichomi.

Pia humsababishia kuvimba kwa kuta za mji wa mimba na kuta za mirija ya uzazi yaani Pelvic Inflamatory Disease (PID). Mwanamke anayesikia maumivu chini ya kitovu katikati na pembeni lakini pia akawa anatokwa na uchafu mzito mithili ya maziwa mtindi, kuna uwezekano akawa na PID hasa kama amewahi kukumbwa na tatizo la kuharibika kwa mimba kabla haijafikisha miezi mitano.

Itaendelea wiki ijayo.


Loading...

Toa comment