×

Virusi vya Corona Vyahofiwa Kutua Afrika

MAOFISA wa afya wanamshuku mgonjwa mmoja nchini Ivory Coast kuwa na virusi vya corona, waziri wa afya ametangaza.

 

Mwanafunzi mmoja, mwanamke, ambaye jina lake halikutajwa, alikuwa ametokea China, mjini Beijing, na kurudi kwao Afrika Magharibi siku yaJjumamosi, sasa anafanyiwa vipimo zaidi baada ya kukutwa na mafua, ambayo ni moja ya dalili za ugonjwa wa Corona.

 

Imethibitishwa kwamba mgonjwa huyo atakuwa wa kwanza barani Afrika kufanyiwa vipimo hivyo vya virusi hatari.

 

Virusi hivyo vilibainika kwa mara ya kwanza katika mji wa China wa Wuhan, na sasa watu 2,000 wana virusi hivyo na 56 wamefariki tayari.

 

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 34, ametengwa kwa sasa, maofisa husika walisema. Mwanamke huyo anadaiwa kuishi China kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, kwa mujibu wa taarifa ambayo ilitolewa na wizara ya afya ya Ivory Coast na kuongeza kuwa alionyesha dalili za mafua kabla hajapanda ndege akiwa anaelekea Abidjan.

 

“Kuna hali ya wasiwasi kuwa dalili alizokuwanazo zina uhusiano na virusi vya corona,” alisema ofisa mmoja.

 

Majibu ya vipimo vya mwanamke huyo yanatarajiwa kutolewa siku ya Jumapili jioni. Kwa sasa virusi hivi vinavyofahamika kama 2019-nCoV, vinadaiwa kuwa maambukizi mapya kwa binadamu. Tangu mlipuko wa ugonjwa huo kuanza Wuhan, mataifa kadhaa ya Afrika yameanzisha vipimo vya kuangalia virusi vya Corona kwa watu wanaotoka China.

Leave a Comment