The House of Favourite Newspapers

MJUMBE AANIKA MAISHA YA LULU

DAR ES SALAAM: Msanii wa Filamu Bongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ ambaye kwa sasa yupo huru baada ya kumaliza kifungo chake Novemba 12, mwaka huu, ameanza maisha mapya ya uraiani kwa kujiachia huku mjumbe wake wa mtaa aliyefahamika kwa jina la Alphonce Joseph akianika maisha yake kwa sasa.

 

Mjumbe huyo amemfungukia staa huyo baada ya waandishi wetu kutinga kwenye mjengo anaoishi kwa sasa uliopo maeneo ya Bahari Beach, Kazima Road jijini Dar kwa lengo la kujua mapya baada ya kifungo cha kesi iliyokuwa ikimkabili ya kumuua bila kukusudia aliyekuwa mpenzi wake, Steven Kanumba kuisha.

 

BREKI YA KWANZA GETINI

Baada ya waandishi kuoneshwa nyumba anayoishi Lulu, walitembea kwa tahadhari kuelekea lilipo geti la kuingilia kufuatia kutahadharishwa kuwa, kuna ulinzi mzito.

Baada ya kulifikia geti lililokuwa katikati ya kuta ndefu zilizoizunguka nyumba hiyo ya kifahari, waandishi walisikia sauti za watu wakizungumza ndani lakini licha ya kugonga kwa muda mrefu hakuna mtu aliyeitika wala kutoka nje.

 

MLINZI ATOKEA NYUMBA YA PILI

Kufuatia waandishi wetu kugonga geti kwa muda mrefu, ghafla alitokea kijana mmoja kutoka kwenye geti la nyumba ya pili ambapo alipoulizwa kama pale ndipo anapoishi Lulu, alikataa kutoa ushirikiano.

“Mimi ndiye mlinzi wa nyumba hii, siruhusiwi kutoa taarifa zozote kuhusu wahusika,” alisema mlinzi huyo kisha akaingia kwenye nyumba anayodaiwa kuishi Lulu na kufunga geti.

 

Zilipopita takribani dakika mbili, mlinzi huyo alitoka tena nje ambapo waandishi waliokuwa bado wanang’aang’aa macho walimuomba awaoneshe kwa mjumbe wa mtaa na bila hiyana kijana huyo akawaelekeza.

“Ni nyumba ile pale mbele, wala hana shida mnaweza kwenda kuongea naye kuhusu huyo mnayemuulizia,” alisema mlinzi huyo.

 

AMANI USO KWA USO NA MJUMBE

Baada ya kumfikia mjumbe wa mtaa huo aliyejitambulisha kwa jina la Alphonce Joseph alikiri kusikia kuwa Lulu anaishi kwenye eneo lake lakini hakuwahi kumtia machoni hata siku moja.

“Huwa namuona tu kwenye TV na kumsikia kwenye redio lakini sijawahi kumuona laivu yeye wala huyo mwanaume wake anayeishi naye, licha ya kwamba sheria zetu zinasema kila mtu anayehamia hapa lazima afike kwa mjumbe ajitambulishe, wao hawakufanya hivyo.

 

“Ila mimi najua pale ndio wanapoishi. Wanaishi maisha flani ya tofauti sana kwa kweli, siyo watu wa kujichanganya kwenye jamii.

“Lakini kwa mfano nikifanikiwa kuonana naye laivu nitamshauri sasa atulie, aangalie maisha yake ili hayo mambo yaliyomkuta yasije yakajirudia tena,” alisema Alphonce.

 

MAJIRANI NAO WAMFUNGUKIA

Baada ya mjumbe kufunguka hayo, waandishi wetu pia walipata fursa ya kuongea na majirani wa Lulu ambapo wengi licha ya kudai anaishi maisha ya kishua, walifungukia jinsi staa huyo asivyojichanganya kwa watu.

 

“Mimi najua Lulu anaishi humu lakini nimewahi kumuona siku moja tu, siyo mtu wa kujianika, mara nyingi anakuwa ndani tu, anaishi maisha flani ya kishua,” alisema jirani mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Fred.

 

Jirani mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Mama Penina alisema: “Yaani ni kwamba hapo ndani hata watoto huwa hawatoki nje, huwa tunawaona ndani ya gari tu wakiwa wanaenda shuleni na kurudishwa, kuna sehemu kubwa tu humo ndani ya kucheza na hadi swimming pool imo sasa watoke nje watafute nini?

 

“Huyo Lulu mwenyewe huwa tunaishia kumuona tu akipita na gari, mama yake ndio huwa anasalimia akiwa amekuja.”

Mwingine aliyekuwa na Mama Penina aliyekataa kutaja jina lake alisema: “Mimi nina mwaka hapa lakini sijawahi kumuona kwa macho yangu zaidi namuona kwenye muvi na simu, kuna mwanangu huwa ananionyesha na kuniambia kuwa huyu dada ndio anayeishi pale kwenye ule mjengo.”

 

TUJIKUMBUSHE

Lulu awali alikuwa akiishi na mama yake maeneo ya Mbezi Beach kabla ya hivi karibuni kuhamia Bahari Beach baada ya kuvishwa pete ya uchumba na bwana wake aliyedumu naye kwa muda mrefu.

Stori: Neema Adrian na Memorise Richard, Amani

BENKI YA DUNIA imeridhia kutoa dola milioni 300 kwa Tanzania

Comments are closed.