The House of Favourite Newspapers

Mtatiro Akamata Tani 10 za Korosho Zilizooza

0

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro ameendesha oparesheni ya mazao wilayani Tunduru kwa siku 2 mfululizo na kufanikiwa kukamata tani 10 za korosho zilizooza za miaka ya nyuma ambazo hazizalishwi wilayani Tunduru.

DC Mtatiro ameiongoza Kamati ya Usalama ya Wilaya yake kufanya oparesheni hiyo baada ya kujulishwa kuwepo kwa njama za baadhi ya wafanyabiashara wenye nia ovu ya kuingiza korosho chafu na zilizooza kwenye soko la korosho bora inayozalishwa wilayani Tunduru.

Kiutafiti Tunduru ndiyo inaongoza kwa kuzalisha korosho tamu zaidi duniani, lakini wako watu wenye nia ovu ambao wamekuwa wakijaribu kutoa korosho mbovu nje ya wilaya hiyo na kuziingiza kwenye soko la Tunduru na matokeo yake hali hiyo ikiachwa itashusha ubora na sifa za kipekee za korosho ya Tunduru.

Mtatiro amesema yeye na vyombo vya usalama vya wilaya yake watafanya kila wawezalo kuhakikisha zao la korosho linalindwa kwa wivu mkubwa na yeyote atakayejaribu kulichezea atakutana na mkono wa dola.

Katika oparesheni ya jana Ijumaa iliyoisha saa 8.30 usiku, jumla ya tani 10 za korosho na watuhumiwa 6 walitiwa mbaroni.

Mtatiro amesema taratibu zote zikikamilika korosho hizo zilizooza na zisizofaa zitateketezwa kwq mujibu wa sheria ili wajanja wasije kuziingiza sokoni.

Idd M. Mohamed, Tunduru.

Leave A Reply