The House of Favourite Newspapers

MTOTO ALIYECHANGIWA NA MONDI… MAZITO YAIBUKA!

DUNIA haina huruma! Licha ya mateso anayoyapata kutokana na ugonjwa wa kansa ya mifupa unaomsumbua, mazito yameibuka kwenye familia ya mtoto Rajabu Omary (20), mkazi wa Isamilo jijini Mwanza baada ya kuzuka kwa tafrani kubwa.  

Mtoto huyo ambaye hivi karibuni alichangiwa fedha kwa ajili ya matibabu na staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ au ‘Mondi’ ameibua hisia za watu wengi ambao wamejikuta wakiguswa na afya yake.

Kampeni ya kumchangia matibabu ilikuwa inaongozwa na Mtangazaji wa Kipindi cha Nitetee kinachorushwa kupitia kituo cha Runinga cha Channel Ten, Flora Lauwo ambapo michango hiyo imesababisha kutokuelewana kati ya familia na mtangazaji huyo na kufikia hatua ya kukunjana mashati.

Chanzo cha kuaminika kilicho karibu na familia hiyo kililiambia Ijumaa Wikienda kuwa baada ya Flora kuitangaza habari ya mtoto huyo, watu wengi walikuwa wakimchangia wakiwemo mastaa mbalimbali kama Diamond, Zari na wengine hivyo kaka wa Rajabu alianza kuingiwa na fikira tofauti na kuhisi kwamba mdogo wake huyo anatumika kwa ajili ya watu kujipatia fedha.

“Yaani baada ya watu wengi kuanza kumchangia mtoto huyu, kaka yake alianza figisu na kukataa asifanyiwe mahojiano yoyote na vyombo vya habari kwa madai kuwa anatumiwa tu ili watu wajipatie fedha hivyo akaanza vita nzito na Flora ambaye alikuwa akichangisha,” kilisema chanzo chetu jijini Mwanza.

Kikiendelea kueleza, chanzo hicho kiliweka wazi kuwa, kaka huyo wakiwa katika Hospitali ya CF iliyopo jijini humo walianza kuzozana mpaka kufikia hatua ya kukunjana mashati na Flora hivyo kusababisha Polisi kuingilia kati na kumkamata kaka huyo wa Rajabu. “Yaani pale hospitalini kuligeuka uwanja wa vita maana yule kaka wa Rajabu hakuogopa hata pale ni hospitalini na kuna wagonjwa kwani alianza kufoka na kukunjana na watu, basi ikawa ni shida tupu,” kilisema chanzo hicho.

RAJABU ARUDISHWA NYUMBANI

Kutokana na purukushani hiyo, uongozi wa hospitali haukufurahishwa na kitendo hicho hivyo uliamua kumpa mgonjwa dawa tu za kwenda kutumia nyumbani kisha kumruhusu. “Kitendo kile hakikuwafurahisha madaktari hata kidogo pale hospitalini maana kilikuwa ni cha aibu sana kwa kweli,” kilisema chanzo hicho.

FLORA AFUNGUKA

Baada ya kupata habari hiyo, Ijumaa Wikienda lilimtafuta Flora ili kuzungumzia madai hayo ambapo alifunguka kuwa, kwa sasa amekuwa kama hayuko sawa kutokana na matatizo hayo aliyoyapata hivyo kuomba aachwe apumzike.

“Yaani hii kazi ninayoifanya ni ya jamii, lakini inahitaji uvumilivu sana maana tunakutana na changamoto kubwa, yaani kiukweli hapa siko sawa, siwezi kuzungumza chochote maana yaliyonipata ni makubwa sana,” alisema Flora. Hivi karibuni Flora alimuibua kijana huyo katika kipindi chake ambaye anateseka kitandani kwa miaka minne akihitaji msaada wa matibabu hivyo watu mbalimbali wakiwemo mastaa nao walishiriki katika kumchangia.

Comments are closed.