visa

Mwanamke kukosa hamu na msisimko wa tendo la ndoa

TATIZO hili la mwanamke kukosa hamu na raha ya tendo la ndoa kitaalam huitwa low sex drive. Tatizo hili huwa halianzi ghafla. Huanza taratibu sana na huchukua miaka mingi hadi kuja kujitokeza. Mwanamke huanza kupata hali hii pindi anapoanza mahusiano ambapo tatizo hujitokeza mwanzoni tu mwa mahusiano hayo au pale mahusiano yanapokwisha au kuvunjika au mume kufariki dunia au kama amepata mabadiliko makubwa maishani ambayo yameathiri afya yake.

Wapo wanawake ambao huwa hawana hamu ya tendo, lakini wakianzwa, hupata hamu, kitaalam tunasema wana msisimko mdogo wa hisia za tendo la ndoa, hali ambayo kitaalam inaitwa hypoactive sexual desire disorder au HSDD.

CHANZO CHA TATIZO

Hamu ya tendo la ndoa misingi yake ni migumu kidogo kutokana na kuhusishwa na mambo mbalimbali yanayohusiana na tendo lenyewe. Hii ni pamoja na hali halisi kiafya, kimwili na kiakili, uzoefu katika tendo hili, imani za dini na mtindo wa maisha unayoishi na uhusiano wako wa sasa. Endapo utakuwa na tatizo katika misingi hiyo, lazima utakuwa na tatizo au utapata tatizo katika tendo la ndoa.

JINSI MATATIZO YA KIMWILI YANAVYOATHIRI

Magonjwa ya muda mrefu au maumivu ya mwili, mabadiliko yasiyo ya kawaida ya mwili, matumizi ya madawa makali ya kutibu magonjwa, huchangia kupunguza hamu na msisimko wa tendo la ndoa kwa mwanamke.

Matatizo ya kimwili kwenye ufanyaji wa tendo la ndoa au sexual problems husababisha maumivu wakati wa tendo la ndoa na kutofikia kileleni. Hali hii huondoa au kupunguza hamu ya tendo la ndoa. Magonjwa au medical deseases husababisha kuondoa na kupunguza hamu na msisimko wa tendo la ndoa. Magonjwa haya ni kama vile magonjwa ya mishipa ya fahamu.

Matumizi ya madawa, mfano dawa za magonjwa ya akili pia huchangia kwa kiasi kikubwa tatizo hili, hasa za ugonjwa wa sonona au depression, ulevi uvutaji wa sigara, madawa ya kulevya huchangia tatizo hili, kwa hiyo ni vizuri kuacha au kupunguza matumizi ya vilevi.

Upasuaji wa matiti au sehemu za siri husababisha kwa kiasi kikubwa tatizo hili, mbaya zaidi ukeketaji, huchangia sana kumuondolea mwanamke hamu na msisimko wa tendo. Kwa hiyo mila ya ukeketaji ni vema ipigwe marufuku. Uchovu wa aina yoyote ile husababisha mwanamke apoteze hamu ya tendo la ndoa.

JINSI MATATIZO YA MFUMO WA HOMONI YANAVYOATHIRI

Mabadiliko katika mfumo wa homoni mwilini endapo yataenda vibaya, basi huathiri uwezo wa tendo la ndoa kwa kukosa hamu na msisimko. Hali hii hutokea wakati wa ukomo wa hedhi kwenye umri mkubwa ambapo kuta za uke husinyaa na kuwa kavu. Hali hii pia huwapata hata wanawake wa umri wa kati. Ujauzito na unyonyeshaji pia huchangia kupunguza kiwango cha homoni zinazosaidia hamu na msisimko wa tendo na mwili kuwa mchovu.

MATATIZO YA KISAIKOLOJIA

Hali hii huathiri akili, mwanamke kusononeka au kuwa na hofu na wasiwasi wa mara kwa mara huchangia kupatwa na tatizo hili. Msongo wa akili au stress kutokana na hali ya maisha na muonekano mbaya wa mwili au sura endapo utajihisi hivyo basi huwezi kupata hamu na hisia.

Mwanamke kutokujiamini kama wewe ni mzuri na una uwezo mzuri wa kushiriki tendo pia inaweza kukuathiri. Mwanamke ambaye tayari alishadhalilishwa kijinsia hupatwa na tatizo hili. Kwa hiyo mwanamke aepuke kujidhalilisha na kudhalilishwa kijinsia kwani athari zake ni kubwa. Kuwa na hisia. Pia endapo ulikorofishana na mpenzi wako aliyepita na mkawa na mgogoro, basi itakuathiri katika mahusiano yajayo.

MATATIZO YA MAHUSIANO

Ukaribu na mpenzi wako hudumisha hamu na hisia za tendo, wanawake wengi hupata tatizo hili la kupoteza hamu na msisimko wa tendo la ndoa kutokana na mahusiano kuvurugika, endapo hakuna mawasiliano mazuri na mpenzi wako, aidha yupo eneo ambalo upo au yupo mbali na wewe, lakini hakuna mawasiliano, kuachana kwa ugomvi, wakati mwingine mnaweza kuwa mnaishi pamoja, lakini migogoro na ugomvi haviishi na wakati mwingine mnapigana kabisa, kutokuwa na mawasiliano ya uhakika au kutokujua na kutofuatilia kwa mwenzi wako endapo wewe unahitaji tendo hilo na kwa jinsi gani au wakati gani, wanawake wengi wanataka wafuatiliwe hivyo na wapenzi wao na wanakuwa wagumu kuanzisha. Katika hili, la mwisho ni kutoaminiana, mwanamke haaminiki au hamuamini mumewe na kuna hisia endapo atashirikiana naye, basi anaweza kupata magonjwa ya viungo vya uzazi, magonjwa ya zinaa au muwasho ukeni na hata Ukimwi.

Itaendelea wiki ijayo.
Toa comment