The House of Favourite Newspapers

Nane Bora Gekul Cup Babati Kuanza Kutimua Vumbi Leo

Mashindano ya Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, Pauline Gekul yaliyopewa jina la Gekul Cup yameendelea kushika kasi huku Hatua ya Nane Bora kwa Mpira wa Miguu ikitarajiwa kuanza kutimua vumbi leo Jumapili katika Uwanja wa Kwaraa mjini Babati.

 

Mashindano hayo yanashirikisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu ambayo ilianzia ngazi ya kata timu zikichuana vikali kusaka bingwa atakaekwenda kuiwakilisha kata yake ngazi ya jimbo, mpira wa wavu, mikono, riadha, kamba, mkuki, pool table, draft na kuimba muziki.

 

Kwa mujibu wa muandaaji wa mashindano hayo Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, Pauline Gekul amesema michuano katika ngazi ya jimbo Hatua ya Nane Bora inatarajiwa kuanza kesho Jumapili na fainali itakuwa ni Julai 27 kwa michezo yote huku akiwaomba wadau wa soka mjini Babati kujitokeza kwa wingi kuzisapoti timu zao na kuzitaka timu pia zije zikiwa zimejiandaa vyema kushindana na siyo kushiriki.

Amesema kwa upande wa mpira wa miguu wamepata timu nane ambazo zimetwaa ubingwa kutoka kata nane za Jimbo la Babati Mjini ambazo ni Mrara FC kutoka Kata ya Babati Mjini, Bonga Mjini FC ya Bonga, Halla FC kutoka Nangara, Malangi FC kutoka Maisaka, Bagara Ziwani FC ya Bagara, Miomboni FC ya Mutuka na Imbili SC ya Sigino huku michezo mingine ya pool table na draft zikiendelea huku mpira wa pete, wavu na kikabu zenyewe nazo zikitarajiwa kuanza kutimua vumbi kesho.

Gekul ametaja sababu kumi zilizomfanya yeye kuamua kuandaa mashindano hayo kuwa ni kutatua changamoto ya vifaa vya michezo, kukuza na kutambua michezo ya kiutamaduni jimboni kwake, kutatua changamoto za vijana wanao jihusisha na muziki, kukuza na kuendeleza michezo ya asili pamoja na kutatua changamoto zao.

Kukuza vipaji vya michezo mbalimbali, kutambua na kukuza jitihada za wanariadha jimboni, kuhakiki michezo mbalimbali na kupata viongozi madhubuti kwa maendeleo ya michezo jimboni,kupiga vita magonjwa yasiyo ambukiza kwa wananchi wa Babati na kujenga umoja wa wana Babati kupitia michezo huku akigusa maisha ya walemavu na wanafunzi wasio jiweza kielimu.

 

Alisema mashindano hayo yatakuwa ni endelevu huku akiweka wazi kuwa mwakani yataboreshwa zaidi kwani ndiyo wameanza hivyo anaamini Jimbo la Babati litaenda sambamba na majimbo mengine yaliyoendelea kimichezo na kuwaomba wadau wa soka na michezo wilayani Babati kuendelea kuwekeza katika sekta hiyo hili jimbo hilo liweze kurejesha heshima yake hasa ya kisoka ambayo kwa sasa imepotea tofauti na miaka ya nyuma.

 

Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama cha Soka Wilaya ya Babati (BDFA) ambao ndiyo wasimamizi wa michuano hiyo, Gerald Mtui amesema kama uongozi wa soka wilaya wanamshukuru mbunge uyo kwa kutambua umuhimu wa michezo kwani kwa kufanya hivyo kuna vipaji vingi vitaibuliwa ambavyo baadae ndiyo zitakuja kuleta heshima ya soka Mkoa wa Manyara huku akiwaomba wadau wengine pia kujitokeza na kumuunga mkono Mbunge uyo.

 

Amesema upande wa zawadi wamepanga bingwa kutoka kila kata atapata jezi seti moja lakini katika ngazi ya jimbo mshindi wa kwanza atapata shilingi laki saba,wa pili shilingi laki tano huku watatu yeye akiondoka na shilingi laki tatu

Habari na Kennedy Lucas, Manyara.

Comments are closed.