The House of Favourite Newspapers

Ntuyabaliwe: Ukiwa na Ndoto, ota Ndoto Kubwa Kupindukia

Jacqueline Ntuyabaliwe Mengi,

MIONGONI mwa vitu ambavyo Hawezi kukwepa mwanamama Jacqueline Ntuyabaliwe Mengi, ni historia yake kwamba aliwahi kuwa Miss Tanzania mwaka 2000, kuwa mwanamuziki aliyefanya vizuri na nyimbo nyingi nzuri, kipindi hicho akijiita K lynn.

Hata hivyo baada ya kuachana na muziki mwaka 2011, alipoolewa na mfanyabiashara mkubwa nchini Reginald Mengi, kwa sasa pia ni mfanyabiashara anayemiliki kampuni iitwayo Amorrete Ltd, kiwanda kidogo huko Mikocheni pamoja na ‘show room’ ya ‘funiture’ iitwayo Molocaho.

Jambo zuri kuhusu Jacqueline, kwa Tanzania huwezi kumtenga pale unapotaja wanawake wanaovutia kwenye jamii hasa kwenye suala zima la mafanikio na kwenye makala hii kwa masaada wa mtandao tutaeleza namna alivyopigania ndoto zake mpaka kufikia mafanikio aliyonayo na utasoma kauli yake juu ya mtazamo wake kwenye mafanikio.

MAISHA YAKE YA UTOTONI YALIKUWA HIVI;

Jacqueline, ni mtoto wa mwisho kati ya watoto watatu wa kike kwenye familia ya marehemu Dokta Ntuyabaliwe, ambapo pia mama yake ambaye amekwisha tangulia mbele za haki alikuwa ni nesi pia.

Ni Muha wa Kigoma aliyekulia jijini Dar es Salaam. Shule ya Msingi na Sekondari amesomea pale Forodhani, chuo amesoma huko Rhodes College, kilichopo London, Uingereza akisoma masomo ya ubunifu. Kuhusu maisha yake ya utotoni Jackline amewahi kuzungumza kwamba, alikuwa ni mtu mwenye aibu na mwenye kupenda kujisomea vitabu kwa kwenda mbele na kusikiliza muziki.

KUHUSU MISS TANZANIA

Mwanamama huyo mwenye miaka 39, kwa sasa amewahi kueleza kwamba masuala ya u-miss yamempa uzoefu mkubwa maishani mwake na hajawahi kujuta kujiingiza kwenye tasnia hiyo.

Alianza kushiriki akiwa kwenye Wilaya ya Ilala, baada ya kushinda alishiriki Miss Tanzania na kushinda pia ambapo alikwenda jijini London, kushiriki Mashindano ya Miss Dunia, yaliyokuwa yanafanyika huko wakati huo. Akiwa huko alijifunza vitu vingi, ikiwa ni pamoja na tamaduni mbalimbali za watu tofautitofauti duniani.

SIKIA SASA KUHUSU MUZIKI

Muziki ndiyo ilikuwa ndoto kubwa ya Jacqueline toka utotoni kwake na amewahi kusema kwamba hakuwa tayari maishani asiitimize ndoto hiyo. Akiwa shuleni hakupenda kuificha, alikuwa akiwaimbia wanafunzi wenzake nyimbo za wanamuziki wa nje.

Baada ya kumaliza masomo, kabla ya Miss Tanzania, alijiunga kwenye bendi iitwayo Tanzanite, alipodumu kwa miaka miwili.Lakini baada ya kushiriki mashindano hayo ya u-miss, aliamua kuachana na bendi na mwaka 2003

ndipo alipoanza muziki rasmi akiwa solo, ambapo alifanya wimbo wake wa kwanza uitwao Nalia Kwa Furaha, aliomshirikisha Bushoke.

Baadaye Jacqueline, alifanya ngoma nyingine kali zikiwemo Crazy Over You aliomshirikisha Squeezer, Chochote Utapata aliofanya baadaye remix na Jay Moe, Nipe Mkono aliomshirikisha Mr Blue na nyingine nyingi.

Hata hivyo mwaka 2011, baada ya kuolewa aliamua kuachana na masuala ya muziki na kwa sasa mwanamama huyu anawatoto wawili mapacha ambao ni Jayden na Lyon.

TUZO NA KUHUSU MAFANIKIO

Mwaka jana Jacqueline kupitia kampuni yake, alipata Tuzo ya Edesign kutoka Italia, taa yake iliyobuni ilivuna tuzo hiyo. Lakini pia alipata tuzo nyingine kutoka ya Bronze kupitia kitu chake alichobuni kiitwacho Ngorongoro Bench.

Kuhusu mafanikio Jacqueline, anasema kwamba mtu yeyote mwenye ndoto anatakiwa kuota ndoto kubwa kupindukia. Mwanamama huyo anasema ingawa ameweza kuwa mwanamuziki kama alivyoota, kuwa mfanyabiashara lakini bado ndoto zake maishani mwake hajazitimiza. Anaamini kupitia kuota ndoto kubwa zaidi ndiyo kutamuongoza mtu kuweza kufikia mafanikio!

Makala: Boniphace Ngumije

 

 

Comments are closed.