The House of Favourite Newspapers

OMMY DIMPOZ AFANYIWA DUA NZITO NA MASHEHE

Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’

KUFUATIA hali yake ya kiafya kuwa mbaya, mwanamuziki wa Bongo Fleva, Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’ amefanyiwa dua ya nguvu na mashehe ili aweze kurudi katika hali yake ya kawaida.  Chanzo makini kilieleza kwamba, mashehe hao walifanya dua hiyo hivi karibuni nyumbani kwa baba wa msanii huyo, Faraji Nyembo mkoani Tabora ili Mungu aweze kumponya na kuwaumbua waliompa sumu.

“Yaani mashehe walifanya dua hapa Tabora, watakuwa waliitwa na baba Dimpoz kwa kuwa anaumizwa mno na hali ya mwanaye kuwa amelazwa huko Sauz (Afrika Kusini) kwa kusumbuliwa na tatizo la mfumo wa chakula kwenye koo,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:

“Unajua haya mambo huenda kuna mambo ya Kiswahili yameingia katika huu ugonjwa na ndiyo maana nasikia wametaka kuwajua kama kuna wabaya wameingiza nguvu zao za kishirikina, basi waumbuke.” Kufuatia mazingira hayo, Risasi Mchanganyiko lilimtafuta baba Dimpoz ambaye alikiri kufanya dua hiyo maalum ili mwanaye aweze kupona haraka. Pamoja na kumuombea apone haraka, pia aliomba kama kuna mtu yeyote alishiriki kumpa sumu Mungu amlipe maana yeye ndiye hakimu wa haki.

“Namuombea sana mwanangu na wale waliompa sumu mwaka hautaisha bila Mungu kufanya kitu kwao. “Naumizwa sana na hali ya mwanangu, natamani ugonjwa unaomsumbua uwarudie haohao waliompa sumu ili waone uchungu wake na wao.

“Ukiangalia mwanangu hana hata mtoto wala mke, bado mdogo, kwa nini wamfanyie hivyo? Aliwakosea nini mpaka wampe adhabu kubwa namna hiyo jamani? “Naamini Mungu atawaweka hadharani siku moja na wataumbuka tu,” alisema baba Dimpoz.

Kwa zaidi ya wiki mbili sasa, Dimpoz yupo chini ya uangalizi wa daktari nchini Afrika Kusini baada ya kwenda kufanyiwa vipimo vya maendeleo ya upasuaji wake wa awali wa koo aliofanyiwa miezi mitatu iliyopita.

Ilibainika kuwa, Dimpoz ana tatizo la nyama kuziba kwenye mfumo wa chakula hivyo baada ya kufanyiwa upasuaji, aliwekewa mpira maalum wa kutolea uchafu ambao hadi mwishoni mwa wiki iliyopita, ilishindikana kuutoa kwa sababu bado kidonda kilionekana kuvuja usaha.

Daktari anayemtibu Dimpoz, alisema tatizo la mfumo huo wa chakula lililompata mwanamuziki huyo lilitokana na kuwekewa sumu kwenye kinywaji. Alisema tatizo hilo limeshawatokea wagonjwa wengi aliokutana nao wakiwa kwenye hali mbaya zaidi, lakini kwa mwanamuziki huyo haikuwa kwenye hatua ya kutisha hivyo kuwa na matumaini makubwa ya kumtibu.

STORI: Gladness Mallya, Risasi Mchanganyiko

Comments are closed.