Polisi Wakana Taarifa za Gari la Polisi Kusababisha Kifo cha Mwananchi Kongowe – Video

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limekanusha vikali taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii, hususan Facebook na Instagram, zinazodai kuwa gari la Polisi lilimgonga mwananchi na kusababisha kifo chake katika eneo la Kongowe wilayani Kibaha, likieleza kuwa madai hayo hayana ukweli wowote.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase tarehe 23 Desemba 2025, ajali hiyo ilitokea tarehe 19 Desemba 2025 majira ya saa 2:00 usiku katika barabara kuu ya Morogoro–Dar es Salaam, eneo la Kongowe wilayani Kibaha, ambapo gari lisilotambulika namba zake za usajili, likitokea upande wa Morogoro kuelekea Dar es Salaam, lilimgonga mwanamke aliyefahamika kwa jina la Pendo Mugisa Mashauri, mwenye umri wa miaka 20, mkulima na mkazi wa Kongowe.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa baada ya ajali hiyo, wananchi walimkimbiza majeruhi huyo katika kituo cha afya cha White Hope kilichopo Miembesaba, Kibaha, ambako alipatiwa huduma ya kwanza kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Tumbi kwa matibabu zaidi. Hata hivyo, majeruhi huyo alifariki dunia tarehe 20 Desemba 2025 majira ya saa 9:00 usiku alipokuwa akiendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo.
“Hakuna shuhuda anayethibitisha kutambua aina ya gari ambalo lilimgonga Pendo Mugisa Mashauri hivyo Jeshi la Polisi linaendelea na msako mkali kuweza kubaini gari lililosababisha ajali hiyo”, imeeleza taarifa hiyo.
Jeshi la Polisi limewataka wananchi kupuuza taarifa zote zinazozagaa mitandaoni ambazo hazijatolewa au kuthibitishwa na mamlaka husika, likisisitiza umuhimu wa kupata taarifa sahihi kutoka kwenye vyombo rasmi.
Video full ipo YouTube ya Global TV
🔴 Tufuatilie kupitia YouTube ya Global TV, like, comment ili kuendelea kuhabarika kila siku kwa habari mbalimbali zenye ukweli na uhakika.

