Samatta: Nimebakiza Kombe la Dunia tu

  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta, amefichua kuwa mpaka sasa amefanikiwa kuweka rekodi za kucheza michuano yote mikubwa katika mchezo wa soka, isipokuwa Kombe la Dunia peke yake.

 

Samatta anayecheza soka la kulipwa katika Klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji, ametoa kauli hiyo baada ya timu yake kuwepo kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ikiwa imepangwa Kundi E na Liverpool ya Uingereza, Napoli ya Italia pamoja na Red Bull ya Austria.

Ikumbukwe kuwa mshambuliaji huyo, msimu uliopita alishiriki Ligi ya Europa huku akiwa na rekodi ya kushinda ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, kushinda tuzo ya mchezaji bora wa Afrika anayecheza ligi ya ndani, kushiriki Kombe la Dunia la Klabu akiwa TP Mazembe kabla ya mwaka huu kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa Afrika ‘Afcon’ akiwa na Taifa Stars.

 

Samatta alisema kuwa kwa upande wake amebakiza michuano hiyo mikubwa peke yake katika mchezo wa soka, kwa kuwa iliyobaki amefanikiwa kushiriki kwa mafanikio makubwa.

“Binafsi naweza kujivunia, siyo kwamba najua sana au vipi lakini ukweli mpaka sasa katika mchezo wa soka nimefanikiwa kutimiza ndoto zangu kwa asilimia kubwa, japokuwa siyo jambo rahisi.

“Unajua baada ya kushinda tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa wanaocheza ligi ya ndani, bado nilikuwa najiona nina deni kubwa juu ya kuweza kutimiza ndoto ya kushiriki michuano ya Afcon, nashukuru nimefanikiwa lakini sasa bado Kombe la Dunia ingawa siyo kitu rahisi kufikia ila ndiyo nilichobakisha kufikia,” alisema Samatta.

SAID ALLY, Dar es Salaam


Loading...

Toa comment