The House of Favourite Newspapers

SIMBA NA YANGA KUKUTANA AGOSTI 23 NGAO YA JAMII, OKTOBA 14 LIGI KUU BARA

0

Ligi Kuu Bara msimu ujao itawakutanisha vigogo Simba na Yanga Oktoba 14 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam lakini kabla, watani hao watakutana Agosti 23, mwaka huu kwenye Uwanja huo, katika mchezo wa Ngao ya Jamii ambao huchezwa wiki moja kabla ya kufunguliwa kwa Ligi Kuu Bara.

Watani hao wa jadi watakapokutana Oktoba, Simba ndiyo watakuwa wenyeji wakati Yanga watakuwa wenyeji katika mechi ya mzunguko wa pili itakayochezwa mwakani ikiashiria kufunguliwa kwa pazia la Ligi Kuu Bara.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas amewaambia waandishi wa habari leo mjini Dar es Salaam kwamba, Ligi Kuu yenyewe itaanza Agosti 26, mwaka huu na kuhitimishwa Mei 20,2018 mabingwa wa Ligi Kuu, Yanga watakutana na washindi wa Kombe la TFF, maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) Agosti 23 katika mchezo wa Jamii na wiki moja baadaye kitimutimu cha Ligi Kuu kitaanza.

Mechi za ufunguzi Agosti 26 zitazikutanisha Ndanda na Azam FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, Simba SC na Ruvu Shooting Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Mwadui FC na Singida United Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga, Mtibwa Sugar na Stand United Uwanja wa Manungu,Turiani, Morogoro, Kagera Sugar na Mbao FC Uwanja wa Kaitaba Bukoba, Njombe Mji na Tanzania Prisons na Mbeya City dhidi ya Majimaji Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Mabingwa watetezi, Yanga wataanza kutetea taji lao Jumapili ya Agosti 27 kwa kumenyana na Lipuli ya Iringa Uwanja wa Taifa, wakati Oktoba 14 watamenyana na mahasimu wao, Simba.

Na Ester Msofe|GPL

Leave A Reply