The House of Favourite Newspapers

Yanga Yaifunika Simba

0
Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi.

KWA mara nyingine Yanga imeifunika Simba kwa gharama za mishahara kwa wachezaji wake wa kikosi cha kwanza ambao wamesajiliwa hadi sasa.

Ukijumuisha wachezaji wapya na wale wa zamani, kikosi cha kwanza cha Yanga kitalipa mshahara wa Sh 41,517,000 wakati Simba italipa Sh 41,400,000. Hapo Yanga imeizidi Simba kwa tofauti ya Sh 117,000 tu.

Gharama hizi za mishahara zinahusu vikosi vya kwanza vitakavyoanza na ambavyo vinatarajiwa kuanza siku zitakapokutana Simba na Yanga, Agosti 19, mwaka huu katika mechi ya Ngao ya Jamii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Donald Ngoma.

NGOMA, NIYONZIMA, OKWI, TAMBWE NGOMA DROO

Raha ya kikosi hicho ni kwamba, nyota wa timu hizo Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Obrey Chirwa wa Yanga na kwa Simba Haruna Niyonzima na Emmanuel Okwi, wote wanapata mshahara mmoja wa dola 3,000 sawa na Sh milioni 6.6.

NINJA, KICHUYA WANAKULA MSHAHARA KIDUCHU

Katika kikosi hicho, wachezaji wanaolipwa kidogo zaidi ni beki wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ aliyesajiliwa kutoka Taifa Jang’ombe, ambaye analipwa Sh milioni 1.

Wengine wanaolipwa kiduchu ni kipa mpya wa Yanga aliyesajiliwa kutoka African Lyon, Youthe Rostand raia wa Cameroon anayelipwa Sh milioni 1.5 na kwa upande wa Simba, Shiza Kichuya analipwa Sh milioni 1.8.

Ibrahimu Ajibu akikabidhiwa jezi yake.

KIKOSI CHA GHARAMA YANGA

Rostand (Sh mil 1.8), Juma Abdul (Sh mil 2.2), Gadiel Michael (Sh mil 2), Ninja (Sh mil 1), Kelvin Yondani (Sh mil 3), Raphael Daud (Sh mil 2), Chirwa (Sh mil 6.6), Thabani Kamusoko (Sh mil 5.5), Ngoma (Sh mil 6.6), Tambwe (Sh mil 6.6) na Ibrahimu Ajibu anayelipwa Sh milioni 4.

Simon Msuva anaondolewa kwenye kikosi hiki, kwani Yanga imekubali kumuuza kwenda Klabu ya Deafer Hassan Al Jadid ya nchini Morocco.

KIKOSI CHA GHARAMA SIMBA

Aishi Manula (Sh mil 2.8), Shomari Kapombe (Sh mil 2.8), Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ (Sh mil 3), Juuko Murshid (Sh mil 2.5), James Kotei (Sh mil 3), Jonas Mkude (Sh mil 5), Kichuya (Sh mil 1.8), Niyonzima (Sh mil 6.6), John Bocco (Sh mil 2.8), Laudit Mavugo (Sh mil 4.5) na Okwi anayelipwa Sh milioni 6.6.

SIMBA YAIFUKUZIA YANGA

Licha ya kuachwa na Yanga kwa Sh 117,000, Simba imeonekana kuongeza gharama katika kikosi chake huku Yanga ikiwa imepunguza kutokana na usajili uliofanyika hadi sasa.

Kikosi cha kwanza cha msimu uliopita cha Simba, hakikufikia jumla ya mishahara ya Sh milioni 30, lakini Yanga ilikuwa zaidi ya Sh milioni 42.

Waliopunguza gharama kwa Yanga ni Ninja anayelipwa Sh milioni 1 akichukua nafasi ya Vincent Bossou raia wa Togo aliyekuwa akilipwa Sh milioni 6.6 pia kipa Deogratius Munishi aliyekuwa akilipwa Sh milioni 2 sasa hayupo na mbadala wake, Rostand analipwa Sh milioni 1.5 tu.

Kwa upande wa Simba walioongeza gharama ni Kapombe na Bocco wanaolipwa Sh milioni 2.8 kila mmoja, Niyonzima na Okwi wanaolipwa Sh milioni 6.6 kila mmoja kwa mwezi.

Mwandishi Wetu | Championi.

Leave A Reply