The House of Favourite Newspapers

Simba Yaagiza Straika wa Kimataifa

MAMBO ni moto Simba! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya uongozi wa timu hiyo kuingia msituni kutafuta bonge la Straika ambaye atakuwa ni moto wa kuotea mbali zaidi ya Mganda, Emmanuel Okwi pamoja na Mnyarwanda, Meddie Kagere.

 

Katika kufanikisha hilo taarifa ambazo Championi Jumatatu limezipata kutoka ndani ya timu hiyo zimedai kuwa uongozi huo chini ya bilionea Mohammed Dewji sasa umeamua kuwapa majukumu mazito baadhi ya mawakala wenye majina makubwa barani Afrika.

 

Mmoja wa viongozi Simba ambaye ameomba hifadhi ya jina lake amedai kuwa mawakala hao wametakiwa kuhakikisha wanampata mshambuliaji huyo ndani ya wiki mbili kuanzia sasa na thamani yake isizidi dola 150,000 (zaidi ya Sh 388 milioni).

 

“Lakini pia awe na rekodi nzuri katika michuano ya kimataifa siyo katika ligi ya kwao tu kama ambavyo ilikuwa kwa Mganda, Juma Balinya ambaye tuliamua kuachana naye kutokana na kutokuwa na rekodi ya kuvutia katika michuano ya kimataifa,” alisema kiongozi huyo na kuongeza kuwa:

 

“Mmoja wa mawakala waliopewa jukumu hilo ni Wakala wa Kagere, Patrick Gakumba ambaye tumekuwa tukifanya naye kazi vizuri.”

 

Alipoulizwa Gakumba kuhusiana na hilo alisema kuwa:“Ni kweli kabisa Simba wamenipatia jukumu la kuwaletea mshambuliaji wa nguvu mwenye CV kubwa katika michuano ya kimataifa.

 

“Kwa hiyo kwa kushirikiana na baadhi ya mawakala wengine pamoja na uongozi wa Simba hivi sasa nipo katika harakati kabambe ya kuhakikisha nashusha jembe la nguvu,” alisema Gakumba.

 

Alipotafutwa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori, ili aweze kuzungumzia hilo hakupatikana kutokana na simu yake ya mkononi kuita tu bila ya kupokelewa.

 

SWEETBERT LUKONGE, Dar es Salaam

Comments are closed.