The House of Favourite Newspapers

Simba Yazidiwa Ujanja na Yanga

UNAKUMBUKA jinsi Yanga ilivyopangua fitna za watani wao Simba kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam? Basi huko Mwanza mikakati thabiti imepangwa, ambapo itakuwa mara mbili zaidi ya ilivyokuwa awali, lengo ni kuhakikisha Mwarabu hatoki.

 

Kama ulikuwa hujui kilichotokea, basi ishu ilikuwa hivi, Simba walijipanga kuujaza Uwanja wa Taifa kwa kuingia mapema tangu asubuhi kwa lengo la kuwashangilia Zesco United ya Zambia katika mchezo wao dhidi ya Yanga hivi karibuni lakini Yanga wakashtukia na kutibua mipango.

 

Inaelezwa kuwa Yanga walitibua mipango hiyo kwa kufika mapema uwanjani siku ya mchezo huo mapema asubuhi na kulijaza jukwaa linalotumiwa na mashabiki wa Simba kwa kukaa wao ili kuwavuruga Wanasimba waliotaka kuwapa wageni nguvu kwa kuwashangilia.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo gazeti hili limezipata na kuthibitishwa na bosi mmoja wa juu klabuni hapo ni kuwa Kamati ya Utendaji ya Yanga imepanga kuwahi kufika Mwanza kwa ajili ya kuweka mipango ya ushindi kwenye mchezo huo.

 

Bosi huyo amesema wamepanga kupangua fitna za Simba walizozipanga kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza watakaoutumia kucheza mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pyramids FC ya Misri kwa kuvamia na kukaa majukwaa watakayokaa watani wao hao.

 

Aliongeza kuwa, pia wamepanga kupeleka jezi 2,000 za Yanga ambazo kuanzia leo Ijumaa zitaanza
kupatikana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba zitakazouzwa na wadhamini wao GSM kwa bei ya shilingi 35,000 na 25,000.

 

“Kama tulifanikiwa kupangua fitna za Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar basi hatushindwi kuzipangua CCM Kirumba, Mwanza mkoa wenye mashabiki wengi wa Yanga.

 

“Hivyo, ni wakati sahihi kwa mashabiki wa Yanga wa Mwanza na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi na mapema ili kuzima fitna za Simba walizozipanga, tumepanga iwe mara zaidi ya tulivyofanya Taifa.

 

“Tunataka uwanja mzima uwe na muonekano wa rangi ya kijani na njano, lengo ni kuwafunga Waarabu nyumbani,” alisema.

Comments are closed.