SportPesa Mambo Ya Sevilla Yalivyo

UJIO wa kikosi cha Sevilla nchini si jambo dogo hata kidogo kwa kuwa tunakubaliana kuwa ni moja ya timu bora na kubwa barani Ulaya. Waratibu wa ziara hiyo ni kampuni maarufu ya kubeti ya SportPesa.

Kama ingekuwa ni Chelsea, Manchester City au Liverpool zinakutana na Sevilla katika moja ya michuano ya Ulaya, basi bila shaka zingejua zina mchezo mgumu. Katika Ligi ya Hispania, maarufu kama La Liga, vigogo Real Madrid na FC Barcelona wanapokutana na Sevilla hata wao wamekuwa wakijua kilicho mbele yao ni kitu kigumu sana na lazima wapambane.

 

Sasa Sevilla itakuwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuwavaa mabingwa wa Tanzania, Simba hii itakuwa ni Mei 23. Siku ambayo ninaamini Watanzania wapenda soka watakuwa na kila sababu ya kujionea tofauti ya radha ya soka la Hispania.

 

Soka la Hispania linajulikana kutokana na kuchezwa kwa utulivu, ubora wa juu na sote tunajua kwamba kama unazungumzia Ulaya ndani ya miaka 10, Hispania ndiyo nchi imetamba zaidi katika soka la Ulaya kupitia klabu zake tatu za Real Madrid, Barcelona na Sevilla ambao ndio wababe wa michuano ya Europa League.

 

Wamewahi kuwa mabingwa wa La Liga mara moja lakini wamewahi kutwaa ubingwa wa Europa League mara tano na ndiyo moja ya timu zilizobeba taji hilo mara nyingi zaidi. Hii maana yake, Sevilla ni moja ya wababe wa Ulaya, jambo ambalo timu nyingi za England ambayo ni ligi maarufu zaidi hazijawahi kufaya.

 

SportPesa ambao wamewahi kuileta Everton FC, moja ya timu zilizoanzisha Ligi Kuu England na kuweka rekodi ya kucheza kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ikiwa na mmoja wa wachezaji bora waliowahi kutoka nchini England, yaani Wayne Rooney, inasema kila kitu kimekamilika.

 

SportPesa ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza michezo nchini na hasa soka, wanaamini ujio wa Sevilla ni nafasi nyingine ya kupiga hatua kwa soka nchini. Mmoja wa maofisa wa SportPesa, Lucas Naghest anasema maandalizi
yamekuwa yakiwapeleka mbio kwa kuwa Sevilla ni timu kubwa na yenye heshima kubwa nchini Hispania katika La Liga pia barani Ulaya.

 

“Ugeni wa timu kama Sevilla hauwezi kuwa mdogo, lakini tunapambana vilivyo kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri. Tuna uzoefu kama uliona michuano ya SportPesa Super Cup, ujio wa Everton na kadhalika. Angalia kuna wachezaji maarufu kama Sol Campbell na wengine wamekuwa hapa.

 

“Tunaendelea kupambana kuhakikisha mambo yanakuwa vizuri na Watanzania watuunge mkono kwa maana kufika uwanjani, waiunge mkono timu ya Tanzania na kujifunza kupitia Sevilla. Muda ungeruhusu tungeomba wacheze mechi mbili au zaidi lakini ni timu kubwa yenye ratiba iliyobana,” anasema.

Kuhusiana na maandalizi, anasema kila kitu kinakwenda vizuri na Sevilla wanaonekana kufurahia kutua Tanzania kwa mara ya kwanza na kuonja ladha ya mpira wa nchi hii. Sevilla watatua nchini siku mbili kabla ya mechi na kuondoka siku hiyohiyo ya Alhamisi baada ya kuivaa Simba kutokana na ratiba yao kuwa ngumu.

 

Simba nao wamekuwa wakijigamba kwamba watafanya vema na kutowaangusha Watanzania kwa kuwa Sevilla watawakuta wakiwa katika fomu kutokana na kuwa wamemaliza ligi muda mchache uliopita na kama hawatakuwa wamemaliza watakuwa ukingoni, hivyo fitnesi yao itakuwa juu na kuwapa nafasi ya kuweza kupambana vilivyo.

 

Mara nyingi kila SportPesa inapotoa nafasi kupitia michuano ya Super Cup, timu za Tanzania zimeshindwa kuitumia kwa kutofanya vizuri lakini safari hii, Simba wamesogezewa tonge mdomoni bila ya jasho na itakuwa kazi kwao, kumaliza kazi.

Loading...

Toa comment