×

Tanzia: Prof. Euphrase Kezilahabi amefariki dunia

Mwandishi mashuri wa riwaya nchini Tanzania, Profesa Euphrase Kezilahabi ameaga dunia. Edmund makaranga Kangi, ambaye ni mpwa wa marehemu, amethibitisha kuwa Profesa Kezilahabi ameaga dunia akiwa jijini Dar es Salaam. Kezilahabi alizaliwa mwaka 1944, alikuwa akifanya shughuli zake nchini Botswana kisha baada ya kuugua alirejea nyumbani Tanzania ambapo alikuwa akipatiwa matibabu.

Profesa Kezilahabi amefariki baada ya kuugua kwa muda mrefu. Profesa Kezilahabi anaelezwa kuwa kielelezo cha aina yake cha uandishi bora, vitabu alivyoviandika vilisomwa sana nchini Tanzania na nje ya Tanzania

Profesa Kezilahabi ni nani?

Prof. Kezilahabi alizaliwa April 13, 1944 Ukerewe, Kaskazini Magharibi mwa Tanzania na kupata shahada yake ya kwanza mwaka 1970 Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alifundisha katika shule mbalimbali nchini Tanzania na baadaye kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, idara ya Kiswahili.

Kisha aliendelea na masomo ya juu katika chuo kikuu cha Wisconsin nchini Marekani. Atakumbukwa kwa kazi zake za uandishi wa vitabu kama vile riwaya ya Rosa Mistika, Nagona, Mzingile, Dunia Uwanja wa Fujo (Riwaya), Dhifa (Ushairi) na Kaptula la Marx (Tamthiliya), Gamba la nyoka na nyinginezo.

Alikuwa mwandishi wa kwanza kuanzisha mapinduzi ya kiuandishi, wenye kuelimisha, kuonya, na kuburudisha pia. Mwandishi mashuhuri wa vitabu nchini Kenya Ken Walibora ameeleza kuwa ”Ulimwengu wa kiswahili umepoteza nguli, mtu ambaye mchango wake ni mkubwa sana kwa jumuia ya wapenda fasihi ya kiswahili na lugha yake”.

”lugha yake aliyokuwa akitumia ni maneno rahisi yenye maana ya kujificha, yana falsafa ya kina kirefu yanayokufanya ufikiri anachokimaanisha” Alieleza Walibora.

Leave a Comment