Tosheka na uliye naye, fanya HIVI akuamini!

MPENZI msomaji wangu, unapoingia katika uhusiano wa kimapenzi na mtu uliyetokea kumpenda sana, awali ya yote unatakiwa kumthibitishia kwamba unampenda kwa dhati, unamuamini, unamheshimu na kumjali.  Weka akilini mwako kwamba, umebahatika kumpata mpenzi ambaye haitatokea siku akaja kukuumiza kwa kukusaliti licha ya kwamba kinyume chake pia yaweza kuwa sawa. Hiyo itakusaidia kuendelea kuishi maisha ya furaha na amani huku ukizidi kulifanya penzi lako kuwa bora kadiri siku zinavyosogea.

Katika kuonesha kwamba una kila sababu ya kujenga mazingira ya kumuamini mwenza wako na unaweza kufanya hivyo, hebu jiulize ni wanaume wangapi ambao wake au wapenzi wao wanagawa uroda nje ya ndoa lakini wao hawajui na wanawaamini kupita maelezo?

Ni wanawake wangapi ambao waume zao ni viwembe ile mbaya lakini wake zao wanawaamini kupindukia na maisha yao yanakwenda sawia? Unadhani ni kwa nini? Hii ni kwa sababu kila mmoja amejenga hali ya kumuamini mwenza wake.

Tutambue tu kwamba, katika maisha ya kimapenzi kuna kitu kuridhika na kutosheka. Unapokuwa na mtu ambaye anakupa kila aina ya furaha maishani mwako bila kuonesha tabia zozote zinazokutia mashaka juu ya penzi lake, huyo mpende, mheshimu na muamini.

Hata kama kuna uwezekano wa yeye kuwa anaficha makucha yake na kuyachomoa pale anapokuwa mbali na wewe, kwa sababu huna uhakika na hujawahi kumuona, chukulia yeye ni msafi kisha yaache maisha yenu yaendelee kuwepo. Nasema hivyo kwa sababu, tukianza kuchunguzana hakuna ambaye ni msafi kwa asilimia mia moja. Kila mtu anajiamini mwenyewe lakini huwezi kuiamini nafsi ya mwenzako kwa asilimia zote.

Ndio maana nikasema, unapoingia katika uhusiano na mtu ambaye umetokea kumpenda sana, ongea na moyo wako! Moyo wako ndio utakueleza kama mpenzi wako ni muaminifu ama sio na pindi utakapoona dalili za kwamba si muaminifu, usimng’ang’anie eti tu kwa sababu umekufa kwake, muache! Nasema muache kwa sababu, kutokuwa muaminifu ni ishara tosha kwamba hana mapenzi ya kweli kwako.

Tatizo tulilonalo wengi ni kutokuwa tayari kuwakosa wale ambao tumetokea kuwapenda sana bila kujua kwamba unaweza kutokea kumpenda mtu lakini yeye akawa hana mapenzi ya dhati moyoni mwake dhidi yako. Ifike wakati basi tukubaliane na uhalisia kwamba, unapoona uliye naye anakuzingua, yupo mwingine mwenye penzi la dhati kwako ambaye anasubiri umuache huyo uliyenaye ili awekeze penzi lake kwako.

Kwa kumalizia niseme tu kwamba, tambua una haki ya kupenda na kupendwa, ukishampata yule unayedhani atayafanya maisha yako yawe ya furaha, mpende kwa dhati na muamini kwamba hawezi kukusaliti lakini, wakati huo hutakiwi kubweteka, chunguza nyendo zake na kama utabaini anajiheshimu, ongeza mapenzi kwake lakini kama utabaini kuwa hajatulia, muache.


Loading...

Toa comment