KAMISHNA wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, amewataka wanachama wa Saccos nchini kuwa mabalozi wa kuhamasisha wananchi kulipa kodi na kutumia mikopo kuanzisha shughuli za kiuchumi zitakazoongeza wigo wa walipa kodi nchini.Amesema, lengo la saccos za watumishi wa umma ni kuwawezesha kiuchumi ili kuongeza ustawi wa kaya na kuhakikisha watumishi wanatimiza majukumu yao kwa uadilifu bila vishawishi vya rushwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya TRA SACCOS LTD, CPA Mbogo Kerenge akizungumza na wanachama wa TRA SACCOS LTD wakati Mkutano Mkuu wa 20 wa Mwaka wa TRA SACCOS LTD iliyofanyika leo Desemba 6, 2025 jijini Dar es Salaam.Aidha, aliwasihi wanachama wote kulinda amani na uchumi wa taifa kwa kuepuka kushiriki au kuunga mkono vitendo vinavyosababisha vurugu na uharibifu wa mali za umma, akitoa pole kwa waliopoteza ndugu au kuumia katika matukio ya vurugu za karibuni.
Kwa upande wake, Naibu Mrajis Mkuu wa vyama vya ushirika wa kifedha CPA Josephat Kisamalala, amesema Saccos imefanikiwa kutoa ajira 10,000 kwa wananchi kwa mwaka 2024, hivyo kuifanya Tanzania kushika nafasi ya tano kwa ubora wa Saccos duniani.
“Kupitia mafanikio haya kumeifanya TRA Saccos kushika nafasi ya tatu na zaidi ya bilioni 90 zimekusanywa kama akiba mwaka 2023, hivyo kuendelea kuchangia pato la taifa na hiyo yote ni kutokana na mazingira mazuri kutoka kwa mwajiri na shauri endeleeni kulinda jina la mwajiri,” amesema Kisamalala.








