The House of Favourite Newspapers

Tshisekedi, Fayulu Walalamikia Dosari Uchaguzi wa Urais Congo

WAGOMBEA wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamelalamikia dosari nyingi wanazosema zilitokea wakati wa uchaguzi wa urais uliofanyika Jumapili.

 

Milolongo mirefu ya wapiga kura ilishuhudiwa katika vituo vingi na mitambo ikafeli kwenye baadhi ya vituo.

 

Aidha, upigaji kura uliathiriwa katika baadhi ya maeneo baada ya mvua kubwa kunyesha, huku baadhi ya wapiga kura wakilalamikia majina yao kutokuwepo kwenye sajili katika baadhi ya vituo.

 

Mmoja wa wagombea wa urais wanaotaka kumrithi Rais Joseph Kabila anayeondoka baada ya kuongoza kwa miaka 17, Felix Tshisekedi, amesema anahofia kwamba huenda hitilafu hizo zilipangwa ndipo kutoa sababu za uchaguzi kufutwa na kumwezesha Bw Kabila kusalia madarakani.

 

Wengi wa wapiga kura walitatizika kutokana na hali kwamba mashine zilitumiwa kwa mara ya kwanza kupigia kura.

Aidha, baadhi ya mashine zilifeli.

 

Bw. John Tendwa, ambaye ni jaji mstaafu nchini Tanzania na aliwahi kuhudumu kama Msajili mstaafu wa Vyama vya Siasa nchini humo amesema iliwachukua baadhi ya wapiga kura hadi dakika saba kupiga kura kituoni.

 

Shughuli ya kuhesabu kura zilizopigwa inaendelea baada ya vituo kufungwa Jumapili jioni na matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa katika kipindi cha wiki moja.

 

Uchaguzi wa sasa ulifaa kufanyika miaka miwili iliyopita lakini uliahirishwa mara kadha kutokana na kutokamilika kwa maandalizi.

 

Kabla ya uchaguzi, kulitokea utata baada ya uchaguzi kuahirishwa katika maeneo yaliyoathiriwa na Ebola yakiwemo miji ya Beni na Butembo mashariki mwa nchi hiyo, na pia katika jiji la Yumbi magharibi mwa nchi hiyo.

 

Hatua hiyo iliathiri takriban wapiga kura 1.26 milioni kati ya jumla ya wapiga kura 40 milioni. Uchaguzi katika maeneo hayo uliahirishwa hadi Machi.

 

Uamuzi huo ulizua utata ikizingatiwa kwamba rais mpya anafaa kuapishwa kufikia katikati mwa Januari.

 

Baadhi ya wanaharakati waliandaa uchaguzi wa mwisho uliopewa jina ‘uchaguzi wa raia’ katika mji wa Goma, mojawapo wa miji iliyoathiriwa, anasema mwandishi wa BBC Gaius Kowene.

 

 

Vituo vya kupigia kura vilifungwa saa kumi na moja jioni, lakini watu waliokuwa kwenye foleni waliruhusiwa kupiga kura.

 

Rais Kabila alipiga kura mapema asubuhi mjini Kinshasa katika shule ambayo mgombea anayemuunga mkono, waziri wa zamani wa mambo ya ndani Emmanuel Ramazani Shadary alikuwa pia anapiga kura.

 

Baada ya kupiga kura, aliambia wanahabari: “Ni wazi kwamba uchaguzi huu ni huru na wa haki, na bila shaka utakuwa huru na wa haki.”

 

Alisema wasiwasi wake pekee ulikuwa kwamba mvua ingeathiri idadi ya watu ambao wangejitokeza kupiga kura.

 

 

Baraza kuu la maaskofu wa kanisa Katoliki (CENCO) lilisema mashine za kupigia kura zilikumbwa na hitilafu katika takriban vituo 544 kati ya 12,300 katika maeneo ambayo walifuatilia upigaji kura.

 

Baadhi ya wapiga kura walilalamika kwamba majina yao hayakupatikana kwenye sajili ya wapiga kura.

 

“Mambo mengi yanakwenda kombo na tunajiuliza iwapo hizi si vurugu zilizopangwa kuhakikisha kwamba kesho mahakama ya kikatiba inafuta kila kitu,” alisema mgombea wa upinzani Felix Tshisekedi.

 

Martin Fayulu, mgombea mwingine wa upinzani, alilalamika katika kikao na wanahabari kwamba sajili za wapiga kura zilitumwa kwa kuchelewa, majina ya baadhi ya wapiga kura yakaandikwa na makosa na kwamba mashine hazikufanya kazi.

 

“Hitilafu hizi zote bila shaka zitaathiri mchakato huu wa leo unaoongozwa na CENI (tume ya taifa ya uchaguzi),” alisema kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.

 

Mkuu wa CENI Corneille Nangaa hata hivyo alisema kwenye runinga ya taifa kwamba shughuli ya upigaji kura iliendelea vyema licha ya kutokea kwa hitilafu ndogo hapa na pale.

Mmoja wa wapiga kura, Fidele Imani, aliambia BBC kwamba aliondoka kituoni baada ya kupiga kura akiwa na matumaini makubwa.

 

“Tumesubiri kwa miaka miwili na nina furaha kwamba nimepiga kura leo,” alisema.

“Tunataka mabadiliko, tunataka amani na tunataka nafasi za kazi.”

Kulikuwa na visa kadha vya ghasia.

 

Watu wawili, polisi na raia, waliuawa eneo la Walungu, Kivu Kusini katika mfarakano uliozuka katika kituo cha kupigia kura, afisa wa UN aliambia BBC.

 

Shirika la habari la Reuters linasema afisa huyo wa polisi alimpiga risasi mpigaji kura baada ya mzozo kutokea kuhusu tuhuma za wizi wa kura, polisi huyo naye akauawa na umati uliokuwa na hamaki.

Kuna wagombea 21 lakini watatu ndio wakuu:

 

1.Emmanuel Ramazani Shadary, Waziri wa zamani wa mambo ya ndani na mtiifu kwa Kabila, ambaye aliwekewa vikwazo na Muungano wa Ulaya kwa hatua zilizochuliwa upinzani wakati wa maandamano ya mwaka 2017.

 

2.Martin Fayulu, Mkurugenzi mkuu wa zamani wa mafuta ambaye ameahidi nchi yenye mafanikio lakini ambaye watu maskini wanahisi hawezi kuwatetea.

 

3.Felix Tshisekedi Tshilombo, Mtoto wa mwanasiasa mkongwe ambaye ameahidi kupambana na umaskini.

Waangalizi wa kanda walifuatilia uchaguzi huo lakini waangalizi wa kimataifa hawakualikwa.

 

Comments are closed.