Kartra

Twaha Kiduku Abeba Gari Baada Ya Kumchakaza Dullah Mbabe

BONDIA Twaha Kiduku amefanikiwa kushinda kwa point dhidi ya Dullah Mbabe katika pambano la uzito wa kati lililofanyika usiku wa kuamkia Jumamosi ya leo Agosti 21, 2021 ndani ya Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salam.

 

Katika pambano hilo alikuwa ni Dullah Mbabe ndiye aliyeanza kwa kasi na kufanikiwa kumpelema chini mpinzani wake katika raundi ya kwanza tu.

Kiduku alienda chini baada ya kupigwa ngumi nzito iliyojaa moja kwa moja usoni.

Baada ya kusimama mwamuzi Njau aliruhusu pambano liendelee ambapo Kiduku alishambuliwa kwa kasi na ilibaki kidogo angepoteza pambano lakini kengele ya kumalizika raundi ya kwanza ikamuokoa.

Kuanzia raundi ya pili Kiduku akaanza kutulia na kurejesha mashambulizi kwa Mbabe.

Ilipofika raundi ya tatu na kuendelea wakawa wanashambuliana kwa zamu lakini alikuwa ni Kiduku ambaye ndiye alionekana kushusha ngumi nzito dhidi ya mpinzani wake.

 

Dullah akawa analazimika kumkwepa Kiduku huku akirusha ngumi za kuvizia.

Mwisho wa pambano majaji wote watatu wakampa ushindi Kiduku ambaye alionekana kuwa mtulivu kuanzia raundi ya tatu hadi ya kumi, pambano lilipomalizika.


Toa comment