The House of Favourite Newspapers

UBAKAJI WANAWAKE USIKU… TELEZA WA KIGOMA NI ZAIDI YA POPOBAWA!

ACHANA na habari za propaganda za popobawa kuwaingilia watu usiku na kuwanyanyasa kingono zilizokuwa zikivuma miaka ya nyuma, sasa kuna kuna watu wanaitwa Teleza; hawa wamekuwa tishio kubwa kwa ubakaji wanawake nyakati za usiku majumbani na kuwajeruhi. Eneo ambalo wabakaji hawa wanatamba na kutishia utu wa wanawake ni mkoani Kigoma hasa Kitongoji cha Mwanga ambapo wanawake wengi wamekiri kufanyiwa unyama huo na kujeruhiwa.

 

TELEZA WALIVYOANZA

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, Teleza ambao hubaka wanawake tu bila kujali umri wao walianza kufanya ukatili huo wa kingono kwa wanawake na watoto wa kike mwaka 2014, lakini taarifa za waliofanyiwa mchezo huo hazikuaminiwa.

“Tangu mwaka 2017 nimeshabakwa mara nne na hawa Teleza lakini nilikuwa nikitoa taarifa kwenye vyombo vya dola vinanipuuza. “Kuna siku walinibaka usiku, asubuhi nilipokwenda polisi kushtaki, cha ajabu askari aliyekuwa ananisikiliza aliniuliza; ‘kwa hiyo Teleza amefanikiwa?’

 

“Nilijisikia vibaya ikabidi nimjibu ‘hajafanikiwa’, hata nilipopewa hiyo PF3 (Fomu ya polisi namba 3 ya matibabu) na kwenda hospitali nako daktari akaniuliza vilevile; ‘wamefanikiwa kukuingilia?’ “Maswali ya namna hii ndiyo yanawafanya wanawake wengi kubakwa na Teleza na kuamua kukaa kimya,” mama mmoja ambaye jina lake tunalihifadhi alimwambia mwandishi wetu na kuapa kujitokeza popote kueleza unyama aliofanyiwa na Teleza.

 

TELEZA WANABAKAJE WANAWAKE USIKU

Baadhi ya wanawake waliofanyiwa unyama na Teleza wanaeleza kuwa awali waliofanya mchezo huo mbaya walikuwa vijana wa kiume lakini hivi sasa wameongezeka na watu wazima nao wanafanya ubakaji huo usiku.

 

“Wakiwa nje wanavua nguo wanajipaka mafuta mwili mzima (Pengine ndiyo chanzo cha kuitwa teleza) halafu wanachukua silaha kama panga au kisu kisha wanavunja mlango na kuanza kukuingilia kimwili, ukiwa mbishi wanakujeruhi, wanaondoka,” mwanamke mwingine alisema.

 

HEBU SIKIA SHUHUDA HII

“Mimi waliingia nyumbani kwangu tena nikiwa nimelala na watoto wangu; kwa kweli nilifedheheka sana, waliniamsha kwanza na baada ya hapo walianza kuniingilia kinguvu mbele ya watoto wangu.

 

“Wakati najitahidi kupambana nao walitoa panga na kunipiga nalo kichwani na kuniacha naugulia maumivu huku watoto wangu wakilia kwa uchungu. “Zamani tulikuwa tukihofia Popobawa ambaye haonekani lakini sasa hivi hawa ni watu kabisa na unawaona, sema ni vigumu kukariri sura zao kutokana na mafuta ya oili chafu wanayojipaka mwili mzima,” alisema mwanamke mmoja aliyekiri kufanyiwa ukatili huo.

 

MWINGINE ASIMULIA ALIVYOJIOKOA

Akizungumza na Risasi Jumamosi, mama mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Sada, alisema kuwa Teleza wawili waliingia nyumbani kwake hivi karibuni usiku na kuanza kumvua nguo kwa nguvu kwa lengo la kumbaka.

“Nilisema kabisa sitakubali; nitapambana nao mpaka mwisho, nilikuwa tayari kufa lakini si kukubali kubakwa kirahisi. “Wakati nakabiliana nao nilikuwa pia napiga kelele, ndiyo mmoja alitoa panga na kunijeruhi nalo shingoni kisha kutoka mbio.

 

MAMA ASIMULIA TELEZA WALIVYOMKATA MKONO

Mama mwingine aliliambia Risasi Jumamosi kuwa, siku mmoja usiku watu hao wabakaji wawili vijana walivunja mlango wa nyumba yake na kuingia ndani kisha kuanza kumlazimisha wafanye naye mapenzi.

 

“Katika maisha yangu sijawahi kukutana na mkasa mzito kama huu wa kusikitisha, kila nikifumba macho yangu naona wazi kitu kibaya nilichofanyiwa mbele ya watoto wangu. “Naiomba Serikali jamani itusaidie sisi wanawake tunadhalilika mno na watu hawa; wanatuachia alama mbaya kwenye familia zetu, we’ unabakwa mbele ya watoto wako kesho mtaangalianaje?” Alihoji mama mmoja ambaye jina lake linahifadhiwa huku akibubujikwa na machozi.

 

ALIYEKATWA PANGA USONI AELEZA MAZITO

Ni kama simulizi ya kwenye sinema lakini ukweli ni kwamba ni matukio ya kweli ambayo wanawake wengi wakiwemo ambao picha zao zimetumika ukurasa wa mbele wamesimulia jinsi Teleza walivyowatendea unyama. Mwanamke mwingine ambaye anakiri kubakwa na Teleza alisema:

 

“Mimi ninachojua na kukumbuka ni lile panga lililopita usoni kwangu na kuingiliwa kinguvu tena na kijana mdogo, yaani ni fedhea iliyopitiliza. “Kinachoniumiza ni kwamba sijui kwa nini nilifanyiwa unyama huu, mtu kukubaka na kukuachia kovu la panga usoni ni ukatili uliopitiliza, kinachosikitisha kingine ni kwamba watu wenyewe hawakamatwi na polisi wakafungwa au kunyongwa.

 

TAMCO WAINGIA VITANI

Muanzilishi wa Shirika lisilo la Kiserikali la TAMCO, Hilda Ngaja linalojihusisha na masuala ya ukatili wanaofanyiwa Wanawake na Watoto, amesema kuwa shirika hilo limejitokeza kupiga kelele kuhusiana na vitendo hivi vinavyofanywa na Teleza. “Tutapambana; tutaandamana mpaka kieleweke, maana hivi vitendo vipo na vinaendelea kuwepo kila kukicha na wanawake ndiyo wanateseka na kupata tabu, inaumiza.

 

“Tunataka serikali itoe tamko, inawalindaje wanawake wa Kigoma na hawa Teleza, hatutakaa kimya na kuacha watu wanabakwa na watoto kuharibiwa sehemu zao za siri,” alisema Hilda ambaye yeye na shirika lake wameshirikiana na mwandishi wetu kujua unyama wanaofanyiwa wanawake.

 

Aidha, Hilda aliongeza kuwa kundi linalojiita Teleza, lilianza kusikika Mkoani Kigoma miaka kadhaa iliyopita na limekuwa likinyanyasa wanawake kingono bila kukomeshwa na vyombo vya usalama.

MKUU WA WILAYA OCD WALALAMIKIWA

Hivi karibuni baadhi ya wananchi wa Kitongoji cha Mwanga walijitokeza kwenye mkutano wa hadhara na kumlalamikia Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Anga na Mkuu wa Polisi Wilaya ‘OCD’ wa Kigoma, SSP Mayunga Mayunga kutokana na tatizo la Teleza.  Bila kujali umati wa watu uliokuwa umefurika mkutanoni baadhi ya wanawake walijitokeza na kumwambia waziwazi mkuu wa wilaya kuwa wao ni waathirika wa Teleza na… kuomba serikali ichukue hatua.

 

Katika mkutano huo mkuu wa wilaya aliwaomba wananchi kutulia na kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola katika kuupiga vita uhalifu huo wa kingono. Naye OCD Mayunga alisema, mtu anaruhusiwa kuua pale anaposhambuliwa kwa lengo la kujilinda na hivyo kuwataka wanawake wanaofanyiwa unyama huo kuwa tayari kuwaua watuhumiwa wanapokuwa wakiwashambulia.

 

Hata hivyo, baadhi ya wanawake waliozungumza na gazeti hili walisema wanamuomba rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, DK. John Pombe Magufuli kulifuatilia suala hili linalodhalilisha heshima ya wanawake. “Mimi namwamini rais akilitolea tamko tatizo hili litakwisha, tumeona mauaji ya Kibiti yamekwisha kwa nini Teleza wasikomeshwe ili wanawake wawe huru kwenye nchi yao.

 

“Kusema kweli hali ni mbaya, hawa wanawake mliowafikia ni wachache mno wapo wengi, watoto walioharibiwa nao ni wengi sana, sasa jambo hili lisichukuliwe kama ni la mchezo ni kubwa,” alisema mama Oscar, mkazi wa Mwanga, alipozungumza na mwandishi wetu.

 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma, ACP Martine Otieno alipohojiwa kuhusu watu hao alisema hao ni wahalifu kama wahalifu wengine. “Nitoe wito kwa wananchi, kama wanawafahamu watu hao watueleze sisi polisi ili tuwafikishe kwenye vyombo vya sheria,” alisema.

Comments are closed.