UKIONA HAYA ,UJUE NI SIKU ZA MWISHO ZA PENZI LENU !

NI Ijumaa nyingine tunakutana kwenye uwanja wetu huu mujarabu wa kupeana elimu ya kuboresha uhusiano wako.  Niende moja kwa moja kwenye mada yangu ya leo inayoangazia ishara mbaya ambazo ukianza kuziona, basi ujue ni siku za mwisho za penzi lenu;

HASIRA MUDA WOTE

Rafiki zangu, kwa mwanamke ukianza kuona mwanaume anakuwa na hasira muda wote na kuhamaki kwenye kila unachokifanya hata kama ni kitu kidogo, unapaswa kujua kuwa  mambo yamebadilika!

Ukiona hivyo ujue kabisa ni kwa sababu penzi lenu limeanza kupungua au kuisha hivyo anakosa uvumilivu kwako. Katika hali kama hii anaweza kukupayukia hata ukiwa katikati ya watu na wala hatajali unavyojisikia kwa yeye kufanya hivyo. Utashangaa na kujiuliza mbona huko mwanzoni aliweza kunivumilia? Jibu ni kwamba penzi limepoa au kuisha.

FURAHA INAYEYUKA

Kwa kawaida mwanaume anavyompenda mwanamke huwa na kiu ya kumfurahisha. Hufanya vitu kuhakikisha mpenzi wake anatabasamu na anajisikia murua. Kila siku kiu ya mwanaume ni kuona mwanamke huyo anatamani kuendelea kuwa ndani ya penzi hilo. Mapenzi yakiisha vitu hivi vyote vinayoyoma na kupeperukia mbali.

KUKOSA MUDA

Ishara nyingine ya mapenzi ya mwanaume yanapokwisha kwa mpenzi wake ni kukosa kabisa kuwa na muda naye.

Mwanzoni mlikuwa mnakuwa na muda wa pamoja, sasa hapati tena muda huo na kila ukiuliza unapewa visingizio kibao. Mara kazi, mara ubize, mara safari, mara kuumwa au kuchoka na kadhalika. Yaani inakuwa ni bora autumie muda wake akiwa na marafiki zake kuliko kuwa na wewe. Vile vicheko vya pamoja mkiwa peke yenu vyote vinakwisha. Ukiona hivyo, ujue hiyo ni taa nyekundu rafiki yangu.

KUACHA KUJALI

Ishara hii yaweza kufanana kidogo na nyingine niliyokwishasema. Mwanaume anapoacha kumpenda mwanamke hupunguza sana au kuacha kabisa kumjali na kumhudumia mpenzi wake. Inakuwa ni ngumu kwake kukufanya ujisikie mwanamke au ujisikie uliye maalum kwake. Atawatendea wengine mema na kuwajali, lakini siyo wewe. Zile bashasha na malavidavi aliyowahi kuwanayo hutoyaona tena!

MAWASILIANO MAGUMU

Mapenzi ya mwanaume yanapopungua au kuisha kwako utaona jinsi inavyokuwa ngumu kwake kuwasiliana na wewe. Unapomwonesha umuhimu au uhitaji wako wa mawasiliano yeye anaona ni mzigo mkubwa. Anakuwa mzito sana kuzungumza, mgumu kuzionesha hisia zake kwako, mara nyingine inakuwia ngumu kugundua lini amefurahi na lini amekasirika. Zamani alikusikiliza, siku hizi hakusikilizi tena. Zamani ulijua alipo na anachofanya siku hizi ukiuliza unazua ugomvi. Ukiona hivi ni dalili kuwa penzi lake kwako linayoyoma.

SIRI NYINGI

Mwanaume anapompenda mwanamke humruhusu mwanamke huyo kuyajua maisha yake yote. Maisha ya mwanaume huyu yanakuwa kama kitabu kilichowazi. Hafichi kitu wala kuishi maisha ya konakona. Tofauti yake ni kwamba mapenzi yakimwisha utaona siri zina kuwa nyingi, haujui nini kinaendelea kwenye maisha yake na wala haoni umuhimu wa kukushirikisha kinachoendelea kinachomhusu yeye.

USHIRIKIANO SIFURI

Penzi la mwanaume linapoisha juu yako mara nyingi huwa anaona shida kukushirikisha kwenye maisha yake au yeye kushiriki maisha yako. Furaha yake inakuwa yake na yako inabaki kuwa yako wakati mwanzoni furaha yako ilikuwa furaha yake.

Ukifanikiwa kitu na yeye anajisikia furaha, lakini siyo sasa. Inapofikia hapa utaona mnakaa nyumba moja kama wapangaji wawili na siyo mtu na mwenza wake. Ukiona mambo haya yanatokea, shtuka, jua hizo ni siku za mwisho za penzi lenu. Nimemaliza, tukutane wiki ijayo!


Loading...

Toa comment