UKIONA YUKO HIVI , JUA ANAKUPENDA KWA DHATI

NI JUMATATU nyingine mpenzi msomaji Mungu ametujalia uzima tunakutana kwenye eneo letu mahsusi kwa ajili ya kupeana elimu ya masuala ya mahusiano. Karibu tujifunze pamoja kama mada inavyojieleza hapo juu.  Dunia ya leo, swali la nitajuaje kama mpenzi niliye naye ananipenda kwa dhati ndilo ambalo huzunguka kwenye akili za watu wengi. Mtu anakuwa na mwenza wake lakini anashindwa kung’amua kama anampenda kwa dhati au la.

WATU WANAISHI KWA HOFU

Watu wengi wanaishi kwa hofu, wanakuwa hawaelewi wenza wao. Bahati mbaya sana, watu wengi kwa sasa wamekuwa waongo. Ni matapeli wa mapenzi, ni vigumu sana kumjua mtu kama anakupenda kwa dhati au la.

Lakini siku zote mimi nimekuwa nikieleza kwenye makala zangu kwamba, mtu hawezi kuwa muongo kwa muda mrefu. Atafanya uongo kwa muda fulani hivyo ukiwa makini utambaini kwamba hakupendi kwa dhati bali yupo na wewe kwa maslahi fulani. Wapo ambao wanakuwa na wewe kwa sababu tu ya maslahi ya fedha. Wao wanakuthamini pale tu wanapokuwa na shida ya fedha. Ni mahodari wa

kunyenyekea wakati huo kuliko wakati mwingine wowote, wakishapata fedha hawana tena habari. Kuna wengine wao wapo kwa ajili ya tendo tu. Anajua kwako akiwa na shida tu ya kufanya tendo la ngono baada ya hapo anakuwa hana mpango na wewe tena. Anakuwa bize na mambo yake, atakutafuta tena atakapokuwa na uhitaji wa ngono.

MAMBO YA KUZINGATIA…

Ndugu zangu, pamoja na ujanjaujanja wa watu wengi walionao lakini kuna mambo ukiyaona kwa mwenza wako ni rahisi kujua kwamba ana mapenzi ya dhati. Mambo yenyewe ni haya yafuatayo:

KUTAMANI KUWASILIANA NAWE KILA WAKATI

Anayekupenda kwa dhati, mara nyingi anakuwa anatamani awasiliane na wewe kila wakati. Anahitaji kukuweka karibu kwa maana ya mawasiliano, ajue upo wapi na unaendeleaje. Ana ile kiu ya kutaka kukujulia hali au kukutana nawe kila wakati. Atakuwa wa kwanza kukutumia ujumbe mzuri wa kukusalimia, anakutakia siku au kazi njema. Anataka kukuona una furaha muda wote.

ANAKUPA KIPAUMBELE

Chochote kile kitakachomtokea kwenye maisha yake, kiwe ni kizuri au kibaya basi wewe utakuwa mtu wa kwanza kukujulisha. Wewe anakuona ndio faraja yake, ndiye mtu ambaye unaweza kuwa wa kwanza kukujulisha akiamini ni mtu pekee unayeweza kulibeba suala lake kwa uzito kuliko mtu mwingine yeyote.

KUJIVUNIA

Anayekupenda kwa dhati anajivunia kuwa na wewe. Haoni aibu kukutambulisha mbele za marafiki zake, anakuwa huru kukutambulisha kwamba wewe ndiye mtu wake. Anatamani kweli marafiki zake wakujue kwamba ndiye chaguo la moyo wake na kwamba amefika, haoni sababu ya kwenda kwingine.

MACHO YANAONGEA

Mtu anayekupenda wakati mwingine sio lazima sana akutamkie anakupenda. Mnapokutana utamuona tu, macho yake yanakuwa na hamu ya kukuona. Anakuangalia kwa kukuhitaji, hata mnapokuwa faragha anaonesha dhahiri kwamba anakuhitaji.

Macho yake yanakiri kukupenda, macho yanazungumza upendo wa dhati. Mtu wa aina hiyo anakuwa kweli anamaanisha anakupenda. Siyo mtu anakuangalia kama hataki. Akikuona ni kama vile tu kakutana na rafiki wa jinsi yake kitu ambacho si sahihi. Kwa leo inatosha, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri!

Instagram&Facebook: Erick Evarist  Twitter: ENangale.

Loading...

Toa comment